Yaliyojiri Leo Mahakamani Kwenye Kesi Ya Abdul Nondo.

Baada ya mahakama kuu kuwaita IGP Simon Sirro, DCI Robert Boaz na Mwanasheria mkuu wa serikali mahakamani kwa ajili ya kujibu kwanini mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia ni mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo hajafikishwa mahakamani, leo Machi 21 ndiyo walitakiwa kufika mahakamani hapo, lakini hawakuweza badala yake waliwatuma mawakili wao kwa ajili ya kuwawakilisha.

Wakiwa Mahakamani hapo viongozi mbalimbali wa mtandao huo, wamezungumza na waandishi wa habari, na kusema kuwa wamepata taarifa kuwa Nondo amesafirishwa kinyemela usiku kupelekwa mkoani Iringa ambapo leo amefikishwa mahakamani, kitendo ambacho wamekilaani kwani ni usumbufu na kwa sababu Nondo alipotelea Dar es Salaam na kwamba kesi yake ilitakiwa kusikilizwa mkoani hapa.

Kwa mujibu wa Wakili wake, Jebra Kambole, amesema dhamana ya Nondo itatazamwa Jumatatu ijayo baada ya hakimu kuomba kusoma sheria inasemaje juu ya kuzuiwa dhamana kwake. Imeelezwa kuwa, Nondo amesomewa mashtaka kwa makosa ya kutoa taarifa za uongo Mitandaoni na kosa la pili ni kudanganya kuwa alitekwa. Shauri limeahirishwa na mtuhumiwa amepelekwa rumande.

Comments