Na Veronica Simba – Kigoma
Wachimbaji
wa Madini wadogo wa Mkoa wa Kigoma, wamemweleza Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli
zao na kumwomba awasaidie kuzitatua.
Walimweleza
changamoto hizo katika kikao maalum, Machi 3 mwaka huu, wakati Naibu
Waziri alipowatembelea akiwa katika ziara ya kazi mkoani humo.
Miongoni
mwa changamoto kubwa waliyoitaja ni kuhusu vibali vya kusafirisha
madini ghafi nje ya nchi; ambapo Naibu Waziri aliwataka kuwa wavumilivu
kwani Serikali inakamilisha mchakato wa kuandaa Mwongozo maalum
utakaopambanua kila aina ya madini yaliyo nchini na yanapaswa
kusafirishwa yakiwa katika hali gani.
“Unajua,
Madini yanatofautiana, na uchakataji wake unatofautiana. Hivyo tumeona
tuandae Mwongozo utakaoondoa mkanganyiko huo na kuwarahisishia kujua
Madini gani yanapaswa kuongezewa thamani kwa kiwango kipi ili uruhusiwe
kuyasafirisha nje ya nchi.”
Alisema
kuwa, Mwongozo huo utatolewa hivi karibuni na hivyo Serikali itaanza
tena kutoa vibali vya usafirishaji Madini nje ya nchi.
Vilevile,
wachimbaji hao walitaja changamoto nyingine kuwa ni upatikanaji wa
Ruzuku ambapo pamoja na kulalamikia Serikali kusimamisha zoezi hilo,
lakini pia walidai kuwa wakati ikitolewa, wahusika hawakutenda haki.
“Wasiokuwa na vigezo ndiyo walikuwa wakipatiwa Ruzuku ilhali wenye vigezo wakinyimwa,” walilalamika.
Akizungumzia
suala hilo, Naibu Waziri aliwaeleza kuwa Serikali iliamua kusimamisha
kwa muda zoezi la utoaji Ruzuku kutokana na kugundua udhaifu katika
zoezi husika ikiwemo baadhi ya wanufaika kutumia Ruzuku waliyopewa kwa
mambo yao binafsi tofauti na masharti yake. Hata hivyo, alisema kuwa
Ruzuku itaanza kutolewa tena baada ya Serikali kujiridhisha kuwa
itatumika vema.
Kuhusu
suala la wenye vigezo kunyimwa Ruzuku na wasio na vigezo kupatiwa;
Naibu Waziri alisema Serikali itafuatilia na kuchunguza kwa ukaribu ili
kuwabaini watumishi wa umma na wengine wanaoshirikiana nao katika
kupindisha utaratibu uliowekwa kwa sababu wanaozijua wao.
“Tukiwabaini
tutawachukulia hatua kali za kisheria. Nanyi tunawaomba mtuletee aina
yoyote ya ushahidi unaoweza kutusaidia kuthibitisha madai yenu ili kwa
pamoja tukomeshe tatizo hilo.”
Aliongeza
kuwa, katika kushughulikia tatizo hilo, tayari Serikali ilishatoa tamko
kuwataka wale waliotumia Ruzuku kwa matumizi binafsi tofauti na
masharti yake, wazirudishe pesa hizo mara moja na kwamba muda waliopewa
kurudisha umekwisha, hivyo wataanza kushughulikiwa.
Wachimbaji
hao pia walilalamikia kutopewa ushirikiano na watumishi wa Ofisi ya
Madini Kigoma ambapo Naibu Waziri aliahidi kufuatilia na kushughulikia
suala hilo.
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza na wachimbaji madini
wadogo wa Mkoa wa Kigoma, wakati wa ziara yake ya kazi mkoani humo,
Machi 3 Mwaka huu.
Katibu
wa Kikundi cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Kigoma, Iddi
Lugundana, akisoma Risala ya Kikundi hicho mbele ya Naibu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati alipowatembelea na
kuzungumza nao, akiwa katika ziara ya kazi mkoani Kigoma, Machi 3 Mwaka
huu.
Baadhi
ya Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Kigoma, wakiwasilisha maoni yao
kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati
alipowatembelea na kuzungumza nao, akiwa katika ziara ya kazi mkoani
Kigoma, Machi 3 Mwaka huu
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Ujumbe wake, wakikagua Kiwanda cha
Kuchakata Chokaa kinachomilikiwa na Kikundi cha Wachimbaji Wadogo wa
Madini Mkoa wa Kigoma, kilichopo Eneo la Simbo, Machi 3 Mwaka huu.
Comments
Post a Comment