UVCCM PWANI YAOMBA VIJANA WENYE VIKUNDI KUPEWA TENDA

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa wa Pwani (UVCCM),Charangwa Selemani Makwiro (katikati) akizungumza na wajumbe wa Baraza la UVCCM la Wilaya ya Kibaha Vijijini leo. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu UVCCM Mkoa wa Pwani,Ramadhan Kapeto na Mwenyekiti UVCCM Wilaya Kibaha Vijijini,Jumanne Mbonde na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Kibaha Vijijini,Murtala Mkumba. Picha zote na Elisa Shunda
NA ELISA SHUNDA,KIBAHA VIJIJINI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha Vijijini imeombwa kuwapatia tenda ndogondogo za ufundi vijana wenye vikundi kama ujenzi wa madarasa,ufyatuaji wa matofali,uchomeleaji wa madirisha au milango au kitu chochote,uaandaji wa chakula katika matukio mbalimbali ya halmashauri ili wajikwamue kiuchumi kwa kuwa uwezo wa kufanya kazi hizo wanao.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani (UVCCM),Charangwa Selemani Makwiro wakati akizungumza na baraza la wajumbe wa umoja wa vijana CCM wa Wilaya ya Kibaha Vijijini katika muendelezo wa ziara yake katika wilaya za mkoa huo ambapo ameweza kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana hao wajasiriamali ambao mitaji yao wamepata kutoka halmashauri hiyo kupitia mkopo vijana wa asilimia 4% unaotolewa nchi nzima kwenye kila halmashauri.
“Kabla ya kuanza mkutano huu nimetembelea miradi mbalimbali ya vijana wa halmashauri ya Kibaha Vijijini nimeona kwa macho yangu vikundi hivyo vya vijana ambapo nimeenda kwenye duka la uuzaji wa unga uliosagwa tayari kwa matumizi,sehemu ya ufyatuaji wa matofali na uchomeleaji,kikundi cha mapambo na mapishi pamoja na kikundi cha ngoma ambacho kinahamasisha na kuburudisha katika shughuli mbalimbali kama kikialikwa kwa bei nafuu,miongoni mwa vikundi hivi vinafanya shughuli zake kutokana na fedha za mkopo ambao wamepewa na halmashauri ya kibaha vijijini hivyo ni jukumu lenu kuwapatia tenda ili wajiendeleze na kujikwamua kiuchumi” Alisema Makwiro
Aidha Mwenyekiti Makwiro amewaeleza vijana hao kuwa halmashauri ya Kibaha Vijijini ipo katika mchakato wa kutenga maeneo kwa ajili ya vijana hao kutumia sehemu hizo kwa ajili ya kufanyia miradi mbalimbali ambazo watazifanya kulingana na mikopo watakayokuwa wamepewa pamoja na kuwakumbusha kutojihusisha na kushabikia jambo lolote linalotaka kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza kwa niaba ya niaba ya Vijana wa Wilaya ya Kibaha Vijijini,Jumanne Mbonde aliahidi kuendelea kushirikiana naye katika kuikwamua Mkoa wa Pwani  na kuwasaidia vijana kufikia malengo endelevu ya kiuchumi ili vijana hao waondokane na fikra mbaya za kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa mbele ya jamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Kibaha Vijijini,Murtala Mkumba amemhakikishia Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Pwani,Charangwa Makwiro akiwa kama mwenyekiti wa wilaya hiyo atakuwa bega kwa began a vijana hao kuhakikisha wanafanikisha malengo yao pamoja na maeneo ya kufanyia shughuli zao za miradi.
Akizungumza katika mkutano huo,Kaimu Ofisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha vijijini,Sophia Msangi alisema kuwa amelipokea ombi hilo la Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Pwani,Charangwa Makwiro la kuwapatia tenda vijana hao wenye vikundi ambavyo vinajishughulisha na kazi mbalimbali na kuahidi kulifanyia kazi

Comments