URUSI NAYO IMEJIBU MAPIGO.....WANADIPLOMASIA 60 WA MAREKANI WATIMULIWA, UBALOZI WAFUNGWA

Urusi imewafukuza wanadiplomasia 60 wa Marekani, na kufunga ubalozi uliopo St Petersburg ikiwa ni majibu kwa kitendo cha Marekani kuwafukuza wanadiplomasia wa Urusi juu ya shutuma ya Uingereza kuhusu kuhusika kwa Urusi katika shambulio la jasusi wa zamani wa Urusi Sergei Kripal na binti yake huko Uingereza.

Hatua hiyo ilitangazwa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov. Zaidi ya nchi ishirini zimewafukuza wanadiplomasia wa urusi nchini mwao katika kuunga mkono Uingereza.

Miongoni mwa nchi hizo ni Marekani ambapo mapema wiki hii iliwatimua wanadiplomasia 60 wa urusi kuondoka Marekani.

Katika kujibu hilo Urusi imewatimua wanadiplomasia 58 kutoka Moscow na wawili kutoka mji wa Yekaterinburg, chombo cha habari cha Interfax kiliripoti.

Lavrov alisema kuwa nchi nyingine zilizowafukuza Warusi wasubiri majibu kwa vitendo.

Ameongeza kuwa Ubalozi wa Marekani umepewa taarifa juu ya hatua hiyo kama majibu kwa Marekani kwa kuwatimua wanadiplomasia wake na kusimamisha ubalozi ulioko St. Petersburg.

Baada ya hatua hiyo msemaji wa Marekani amesema kuwa Urusi haina nia ya kuwa na uhusiano mzuri na nchi nyingine, na hivyo Marekani ina haki ya kuchukua hatua nyingine dhidi ya Urusi.

''Urusi imeamua kujitenga zaidi yenyewe, tunaangalia maamuzi ya kuchukua'' Heather Nauert aliwaambia waandishi wa habari.
 
Urusi imekataa kuhusika kwa namna yoyote na jaribio la mauaji kwa jasusi wake wa zamani. Kripal bado yupo katika hali mbaya hospitalini lakini Binti yake anaendela vizuri na ameondoka katika hali ya hatari.

Kutokana na kuhusishwa kwa Urusi na tukio hilo mapema Uingereza ilisema kuwa hawatatuma mawaziri wake pamoja na familia ya Malkia kushiriki kombe la dunia.

Itakumbukwa kuwa mwaka 1986 Rais wa Marekani Ronald Reagan aliwatimua wanadiplomasia 80 wa Urusi.

Na mwaka 2016 uongozi wa Barack Obama uliwafukuza wanadiplomasia 35 kutokana na kudukua chama cha Democratic.

Credit:BBC

Comments