Wakuu wa nchi zaidi ya 26 kutoka bara la Afrika wamekutana jana Jumatano katika jijini la Kigali- Rwanda, kuhudhuria sherehe za utiaji saini mikataba mitatu ya kisheria kuelekea kuwa na biashara huria.
Miongoni mwa mikataba iliyotiwa saini ni pamoja na azimio la kigali linalozitaka nchi wanachama kujikita kukwamua uchumi wa mataifa yao, itifaki ya uhuru wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine pamoja na mkataba wa biashara huria kwa bara la Afrika CFTA.
Licha ya kuwa baadhi ya nchi hazikutia saini mkataba wa biashara huria, nchi zaidi ya 20 zenyewe zimetia saini kuridhia mkataba huu ambao utaanza kazi pale nchi zote zitakapouridhia. Miongoni mwa nchi ambazo hazijatia saini mkataba huu wa kibiashara ni pamoja na Nigeria ambayo imesema inahitaji kufanya mjadala zaidi kabla ya kutia saini.
Jumla ya nchi 44 zimetia saini mkataba wa biashara huria kwa bara la Afrika wakati nchi 41 zikitia saini mkataba wa azimio la Kigali na nchi 27 zikitia saini itifaki ya uhuru wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Viongozi wa Afrika wanasema hatua iliyofikiwa juma hili ni ya kihistoria katika kufikia bara la Afrika wanalolitaka hasa kwa kuwa miongoni mwa bara lenye uchumi wenye nguvu na ushindani na mataifa mengine.
Kwa mujibu wa takwimu za kituo cha kimataifa cha biashara, mwaka 2012 biashara za ndani ya Afrika zilikuwa kwa asilimia 12 na huku hivi sasa ikikadiriwa kuwa bara hili linafanya biashara kwa zaidi ya asilimia 16.
Tume ya uchumi ya umoja wa Mataifa kwa bara la Afrika inakadiria kuwa ifikapo mwaka 2022 mkataba huu utakuwa umeliwezesha bara la Afrika kufanya biashara kwa zaidi ya asilimia 52 ambayo ni sawa na dola za Marekani bilioni 35.
Wataalamu wanasema miongoni mwa faida za CFTA ni pamoja na kuongeza soko la bidhaa za Afrika, kuboresha na kuongeza kasi ya ufanyaji wa biashara za ndani, kuvutia wawekezaji wa nje, kuwa na soko pana, kurahisisha masuala ya usafirishaji na kuhamasisha ukuzaji wa viwanda.
Comments
Post a Comment