Kurejeshwa Kwa Wasichana Waliotekwa Na Boko Haram Kwawafurahisha Wazazi.


Serikali ya Nigeria imethibitisha kuwa wengi kati ya wanafunzi wa kike 110 waliokuwa wametekwa na kikundi cha Boko Haram zaidi ya mwezi mmoja uliopita wameachiwa jana Jumatano asubuhi.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa wasichana hao walifikishwa katika mji wa Dapchi unaopatikana upande wa Kaskazini mwa Nigeria katika Jimbo la Yobe baada ya wale waliokuwa wanawashikilia kuwarejesha katika msafara wa magari 9.
Taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari zimesema wasichana watano kati ya hao walikufa wakati wakisafirishwa, ingawa afisa wa serikali wa jimbo la Yobe amesema hili bado halijaweza kuthibitishwa.
Naye Waziri wa Habari wa Nigeria Lai Mohammed amesema kuachiwa kwa wasichana hao mapema asubuhi bila masharti yoyote kwa serikali kulitokana na juhudi za kisiri zikisaidiwa na baadhi ya marafiki wa nchi hiyo.
“Wengi kati ya wasichana hao, wengi wa wanafunzi hao walioachiwa huru hawakuletwa wote sehemu moja. Waliachwa njiani na wao wenyewe walirudi majumbani kwa wazazi wao.” Aliongeza Waziri huyo.
Wazazi ambao hapo awali walikuwa wanamsiba kwa kutekwa kwa vijana wao hivi sasa wanasheherekea kurudi kwao.

Comments