MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AWASILI NCHINI AFRIKA KUMUWAKILISHA RAIS DKT MAGUFULI MKUTANO WA 37 WA SADC
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
amewasili nchini Afrika ya Kusini tayari kwa kuhudhuria Mkutano wa 37 wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
SADC unaoaanza tarehe 19 na 20 ambapo kesho tarehe 18 atahudhuria
Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Troika Mbili ya SADC (SADC Double Troika Summit).
Mheshimiwa
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amepokelewa na Waziri wa Mawasiliano
wa Afrika Kusini Mhe. Ayanda Dlodlo akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli.
Akizungumza
mara baada ya kuwasili kwa Makamu wa Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augastine Mahiga amesema
Mkutano huo utapokea na kujadili ajenda mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa SADC na Uchaguzi wa Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na
Usalama; Hali ya Michango mbalimbali ya Nchi Wanachama na Kupokea
taarifa ya Mwenyekiti anayeondoka wa SADC Organ.
Pia
Mkutano utapokea taarifa ya Katibu Mtendaji wa SADC; Kupitia hali ya
kiuchumi katika Kanda ya SADC; Kuwasilisha Kaulimbiu ya Mkutano wa SADC;
Taarifa kuhusu Mfuko wa Maendeleo wa SADC; Taarifa ya Utekelezaji wa
Mpango Mkakati wa Viwanda; Kuwezesha Chuo cha Elimu ya Sayansi na
Teknolojia; Maombi ya Serikali ya Comoro na Serikali ya Burundi kujiunga
na SADC; Utekelezaji wa Mabadiliko ya Kitaasisi ya Umoja wa Afrika na
Mkutano wa Mshikamano kati ya SADC na Saharawi ya Magharibi.
Dkt.
Mahiga amesema katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali
wa Troika Mbili ya SADC (SADC Double Troika Summit) Tanzania itakabidhi
nafasi ya Uenyekiti kwa Mwenyekiti mpya.
Double
Troika inahusisha nchi wanachama sita ambao kwa sasa ni Swaziland,
Tanzania, Afrika Kusini, Angola, Botswana na Msumbiji. Katika mkutano
huo Mfalme Mswati III wa Swaziland atakuwa ndiye Mwenyekiti. Ajenda kuu
katika Mkutano huu ni kupokea na kujadili taarifa kuhusu hali ya
kisiasa, kiulinzi na kiusalama katika Kanda na hasa nchini DR Congo na
Lesotho.
Comments
Post a Comment