Na Jumia Travel Tanzania
Kutokana
na maendeleo ya sayansi na teknolojia binadamu waliyonayo kwa sasa si
jambo la kushangaza kumuwezesha mtu akafanya shughuli zako zote akiwa
yupo sehemu moja ndanin ya muda mfupi.Kwa mfano, kwa kutumia simu yako
ya mkononi unaweza kutatua changamoto kadhaa hapo nyumbani kwako kama
vile kufanya miamala ya fedha kutoka benki na kisha kutoa kwa mawakala
huduma za fedha, kulipia umeme, kulipia maji, kulipia king’amuzi,
kuagiza chakula, kuagiza usafiri, kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma
mbalimbali.Lakini swali ni kwamba, je ni watanzania wangapi wanaiona
fursa hiyo iliyoletwa na teknolojia kama suluhu za changamoto tofauti
zinazowazungukaJibu ni kwamba ni watu wachache sana walioyapokea
maendeleo yaliyoletwa na teknolojia na kuyatumia katika kurahisisha
maisha yao ya kila siku. Ni jambo la ajabu kuona kwamba mtu ameishiwa na
umeme nyumbani kwake lakini hana suluhu yoyote zaidi ya kwenda kwa
mawakala wa huduma za malipo wakati yeye mwenyewe anao uwezo wa kufanya
hivyo kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Zipo
sababu kadha wa kadha zinazopelekea watu wengi kushindwa kuzitumia
huduma hizi ipasavyo mojawapo ikiwa ni elimu ya kuweza kuitumia mifumo
na programu hizo. Ila kwenye suala la elimu sidhani kama ni hoja ya
msingi kwa sababu mifumo takribani yote ni rahisi kwa mtumiaji na
kikubwa zaidi ni kwamba ukiwa unaitumia mara kwa mara inazoeleka kwani
hakuna kinachobadilika.

Kampuni
ya Jumia ambayo imejikita kwenye masuala ya biashara kwa njia ya mtandao
barani Afrika katika nyanja za hoteli na usafiri, manunuzi ya bidhaa,
kazi, makazi, magari, chakula na matangazo mbalimbali imetimiza miaka
mitano (5) tangu kuanzishwa kwake.
Katika
maadhimisho ya sherehe hizo kampuni hiyo imekuwa ikifanya mikutano kwa
njia ya ‘video za moja kwa moja’ na wataalamu na waasisi wa makampuni
mbalimbali ya kiteknolojia duniani. Lengo kubwa likiwa ni kupata
ushauri, uzoefu na mitazamo juu ya ukuaji wa sekta hiyo na mustakabali
wake barani Afrika.
Mojawapo ya wageni walioalikwa kwenye mfululizo wa ‘video’ hizo alikuwa ni Afisa Mtendaji Mkuu na mwasisi mwenza wa
Andela,
Bw. Jeremy Johnson ambayo ni kampuni iliyoanzishwa kwa madhumuni makubwa
ya kuwafunda watengeneza program barani Afrika (Softwarfe Developers)
na kisha kuwaunganisha na makampuni yenye uhitaji wa wataalamu hao.
Mpaka hivi sasa Andela imefungua matawi yake katika nchi tatu ambazo ni
Nigeria (Lagos), Kenya (Nairobi) na mapema mwaka huu waliongeza tawi
lingine jijini Kampala, Uganda.
Bw.
Johnson katika mazungumzo yake na wafanyakazi wa Jumia alieleza kwamba
mojawapo ya vigezo wanavyoviangalia mpaka wanafikia hatua ya kufungua
tawi nchi husika ni baada ya kufanya utafiti wa kutosha wa maendeleo ya
teknolojia pamoja na shauku ya wananchi wa eneo husika katika kuitumia
ili kutatua changamoto mbalimbali za maisha yao ya kila siku.
Hoja ya
msingi iliyoainishwa na mwasisi huyo ambayo Jumia Travel imeibaini
katika mazungumzo yake ni utayari na shauku ya watu kutumia teknolojia.
Kwa hoja hiyo kwa haraka haraka tunaweza kuona kwamba nchi za Nigeria na
majirani zetu wa Kenya wametuacha hatua kadhaa katika kuyapokea
mabadiliko ya kiteknolojia na kuyatumia ipasavyo. Na suala hilo ni
mojawapo ya sababu zinazopelekea makampuni kadhaa kuanzia katika nchi
hizo kabla ya kuvuka mpaka na kuja nchi nyingine ikiwemo Tanzania.
Imefikia
mahali sasa watanzania kubadilika na kuyapokea mabadiliko yanayoletwa na
teknolojia hususani mtandao wa intaneti katika kurahisha maisha yetu ya
kila siku. Zipo huduma nyingi ambazo unaweza ukazipata kwa kubonyeza tu
vitufe vya simu yako mahali popote ulipo na ukazipata.
Tukumbuke
kwamba mabadiliko haya yote huja kwa malengo ya kufanya shughuli zetu
ziwe rahisi tofauti na awali na ndiyo maana watu wanaendelea kufanya
uvumbuzi kila kukicha.
Comments
Post a Comment