Mkapa Awataka Watanzania Waache Kulialia na Kulaamika

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amewataka Watanzania, wakiwamo wanasiasa, kuacha kulalamika kwa kukosekana kwa haki, huku akiwataka kujiuliza iwapo wametimiza wajibu wao.

Amesema amekuwa akichukizwa na baadhi ya wanasiasa hapa nchini, ambao kila siku wamekuwa wakilalamika kutaka haki, hali ya kuwa wao hawatimizi wajibu.

Rais huyo mstaafu ametoa kauli hiyo huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi wa upinzani kudai haki ya demokrasia na kupinga kuzuiwa kufanya shughuli zao za kisiasa kupitia mikutano.

Hatua hiyo imekuwa ikizua malalamiko ikiwemo kuwaomba marais wastafu kujitokeza na kumshauri Rais Dk. John Magufuli kutokana na maamuzi yake mbalimbali aliyoyachukua kwa nchi.

Kutokana na hali hiyo, Mkapa amewataka wasomi na wafanyakazi kuendesha midahalo na makongamano ya kuhakikisha nchi inajitegemea badala ya kulalamika kila siku.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Itilima, mkoani Simiyu, alipokuwa akikabidhi Jengo la Upasuaji (Theater) katika Kituo cha Afya Nkoma, lililojengwa na Taasisi ya Mkapa Foundation kwa gharama ya Sh milioni 270.
 
Rais huyo mstaafu alisema wanasiasa hao, licha ya kulalamika, lakini hawatimiza wajibu wa kuhakikisha wanafanya kazi ili kuletea nchi maendeleo.

Katika kile kinachoonekana kuchukizwa na hali hiyo, Mkapa alisema kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha taifa linajitegemea na kuwaletea wananchi wake maendeleo.

“Kila siku utasikia watu wanadai haki, makongamano, midahalo ya kudai haki, swali la kuwauliza wao je, wametimiza wajibu kama Watanzania… maana hakuna haki bila wajibu, ni lazima kubadilika na kuendesha makongamano ya kuonyesha nchi itajitegemea vipi,” alisema Mkapa.

Rais huyo Mstaafu alisema ili kuweza kujitegemea, ni lazima kila Mtanzania atimize wajibu wa kufanya kazi kama Rais Dk. John Magufuli anavyosema, huku akitoa mfano katika nchi ya Japan ambapo wananchi wake jambo la kwanza ni kufanya kazi.

“Kama tunatarajia mataifa kuja kutuinua wakati sisi tumekaa ni dhana potofu, viongozi tubuni miradi ili tujiendeleze na kujiletea maendeleo sisi wenyewe, kama nchi ya Japan wanavyofanya,” alisema Mkapa.
 
Aliongeza kuwa, toka utawala wa Baba wa Taifa na sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), tangu enzi ilikuwa ni ujamaa na kujitegemea, jambo ambalo ameeleza lazima litekelezwe kwa kila mmoja katika kutimiza wajibu kwa nafasi yake.

Akizungumzia jengo hilo, Mkapa aliishukuru Japan, ambao walitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo kupitia Taasisi ya Mkapa Foundation, lengo likiwa ni kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.
 
“Nchi yetu bado tunakabiliwa na changamoto ya vifo vya akina mama wajawazito pamoja na watoto wachanga, nchi ya Japan wametoa msaada huo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hii.

“… taasisi ya Mkapa itaendeleza ushirikiano na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za afya,” alisema.
 
Baada ya kukabidhi jengo hilo la upasuaji, Rais Mkapa na msafara wake walielekea wilayani Chato

Comments