IRINGA HAPATOSHI, 441 WAJITOKEZA KUWANIA NAFASI MBALIMBALI CCM

Image result for KATIBU WA CCM MKOA WA IRINGA CHRISTOPHER

WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) 441 wamerejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi mkoani Iringa katika uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, huku kukiwepo na tetesi za wagombea mapandikizi kutoka vyama vya upinzani.
Wakati wanachama 100 wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuwakilisha mkoa huo, wanachama 331 wamejitokeza kuwania nafasi hizo katika wilaya nne za kichama za mkoa wa Iringa, Mufindi, Kilolo, Iringa Vijijini na Iringa Manispaa.
Akizungumza na wanahabari leo Jumatano, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Christopher Magala alisema wagombea 13 wamejitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Mkoa huku 12 wakiwania nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu ya Taifa na 15 nafasi ya Katibu wa Itikadi Siasa na Uenezi mkoa.
Waliojitokeza kuwania nafasi ya mwenyekiti ni pamoja na mwanaharakati wa mazingira mkoani Iringa ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Iringa inayomaliza muda wake, Godfrey Mosha.
Mosha ametupa karata yake hiyo kwa mara ya pili baada ya kuangushwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu katika uchaguzi wa mwaka 2012 kwa tofauti ya kura 17.
Wengine ni pamoja aliyekuwa Katibu wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, George Mlawa, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilolo anayemaliza muda wake, Seth Motto na Evans Balama aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali ikiwemo ya Mbeya.
Wengine ni Ephraim Mhekwa, Listen Mpesa, Yusitino Mdesa, Daniel Kidava, Albert Chalamila, Joseph Luwahgo, Yohanes Kaguo, Ramadhani Msigwa na Kelvin Robert.
Kwa upande nafasi moja ya mjumbe wa halmashauri ya kuu ya Taifa aliyejitokeza ni Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Iringa Salim Abri, Mjumbe NEC Mufindi na mjumbe wa NEC Iringa Manispaa, Mahamudu Madenge.
Wengine ni Adestino Mwilinge, Asadi Kikunile, Mgabe Kihongosi, Thom Masini, Enock Ugulumu, Evans Balama, Godfrey Mgongolwa, Obeid Malima na Michael Mlowe.
Kwa upande wa Katibu wa Itikidi Siasa na Uenezi, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa aliwataja waliojitokeza kuwa ni pamoja na Asad Kikunile, Mwinyikheri Baraza, Michael Mlowe, Denis Lupala, Ibrwahim Ngwada, Joseph Mgongolwa, Ally Msigwa, Josia Kifunge, Thadeus Tenga, Pius Njechele, Thobias Kikula, Andre Gemela, John Kiteve, Nasho Kayoka na Godfrey Mosha.
Magala aliwataka wagombea hao kuwa watulivu wakati wakisubiri vikao vya juu kuchuja majina yao na kuzingatia kanuni zinazowazuia kwa namna yoyote ile kufanya kampeni  kabla ya mchujo huo.
Wakizungumzia wagombea hao pamoja na wale waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika ngazi ya wilaya, baadhi ya wanachama wa CCM waliomba vikao vinavyohusika kuwa makini katika kufanya mchujo ili wapatikane wagombea wanye nia njema na chama hicho.
“Kuna baadhi ya wagombea kwa mfano katika Manispaa yyetu ya Iringa kuna wagombea ambao wana damu ya upinzani, wakipita na wakachaguliwa inaweza kuhatarisha shughuli za chama,” alisema mmoja wa wana CCM aliyejitambulisha kwa jina la George wa kata ya Makorongoni.
Alisema zipo taarifa zisizo rasmi zinazozungumzwa katika maeneo yasio rasmi kwamba baadhi ya wagombea waliojitokeza wameshawishiwa na vyama vya upinzani kama mkakati wao wa kuendelea kuihujumu CCM mjini Iringa na mkoani kwa ujumla.

Naye Peter Makongwa wa kata ya Kihesa alisema CCM mkoani Iringa inahitaji viongozi wenye uwezo na nafasi ili kukabiliana na nnguvu ya upinzani hasa katika jimbo la Iringa mjini ambalo CCM waliangushwa vibaya katika chaguzi mbili zilizopita za udiwani na ubunge.

Comments