WIZARA YAKANUSHA TAARIFA ZA GAZETI LA HABARILEO KUHUSU TAKWIMU ZA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI WILAYANI NKASI, RUKWA


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakanusha taarifa zilizoandikwa na gazeti la HABARILEO toleo la tarehe 19 Juni, 2017, kwamba wasichana 2,892 waliokuwa wanafunzi wa shule za msingi wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa walikatishwa masomo yao kutokana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni kwa kipindi cha mwaka 2016.  
 
Taarifa sahihi aliyoitoa Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Bi. Mary Siyame, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu, ni “kwamba kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2016 jumla ya watoto 9,723 waliandikishwa shule, wavulana wakiwa 4,806 na wasichana 4,917 katika wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa. Kwa kipindi hicho (2010-2016) wavulana 2,991 waliacha masomo na wasichana 2971, kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro, kuhama, kupata mimba na ndoa za utotoni.

Aidha, kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Juni 2017 wasichana 8 wanafunzi wa shule ya msingi na wasichana 22 kwa upande wa shule za sekondari walikatisha masomo yao kwa sababu ya kupata mimba na ndoa za utotoni.

Kufuatia taarifa hii, Wizara inasahihisha taarifa ya gazeti la HABARILEO ili kuondoa mkanganyiko unaoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya takwimu zisizokuwa sahihi kuhusu idadi ya wasichana waliokatisha masomo kutokana na mimba na ndoa za utotoni katika wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa kwa kipindi cha mwaka 2016.

Ifahamike kuwa miongoni mwa shabaha kuu za Serikali nchini ni kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kutokana na kupata mimba kwa asilimia 50  ifikapo Juni 2022, kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 27 hadi asilimia 5, na kuongeza msaada wa kielimu kwa wasichana wanaotoka katika familia maskini kutoka asilimia 23.4 hadi asilimia 53.4.

Aidha, Wizara kupitia kitini cha Malezi kwa Familia itaendelea jitihada za kutoa elimu ya malezi kwa wazazi, sambamba na kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Dhamira ya Wizara ni kuona kuwa wadau katika ngazi zote tunashiriki kuzuia mimba na ndoa za utotoni ili kuimarisha upatikanaji wa fursa ya elimu, ulinzi na malezi bora kwa watoto wetu wa kike wakiwemo watoto wa wilaya ya Nkasi na maeneo nchini.  

Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
23/6/2017

Comments