Wauaji wilayani Kibiti wadaiwa kutuma ujumbe kuwa wataendelea kuwauawa Polisi kwa sababu huwadhulum

Siku mbili tangu kuuawa kwa polisi wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani ambao walikuwa kazini katika Kijiji cha Bungu B, hali ya wasiwasi imezidi baada ya wauaji hao kusambaza ujumbe unaoeleza kuwa wanaendelea kusaka askari kwa kuwa ni wadhurumaji.

Watu hao wametuma ujumbe mfupi uliondikwa kwenye karatasi na kisha kuutuma katika mitandao ya kijamii, ukidai kuwa waliouawa (japo hawajatajwa majina yao) walidhulumu watu kwa kutumia kazi zao.

Tunawatangazia wananchi tumewaua hawa kwa sababu wanadhulumu watu kwa kutumia kazi zao na yeyote atakayefanya kazi hapa au nje ya hapa tutamtafuta hata nyumbani kwake. Sisi tumejitolea kufa kuliko kuishi, kwa hiyo dereva au raia popote uwaonapo toa taarifa iwe nyumbani au kazini,” unasema ujumbe huo.

“Hakuna njia ya kumaliza dhuluma isipokuwa chuma tu, hapa chuma tuuu!”

Ujumbe huo ambao umeandikwa kwa mkono kwa kutumia kalamu ya rangi ya bluu unadaiwa kuwa unazungumzia vifo vya askari polisi wawili wa Kituo cha Polisi Kibiti, Sajent Salum na PC Masola waliouawa kwa kupigwa risasi wakiwa kazini.

Mmoja wa madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti (jina tunalo) alisema ujumbe huo unawalenga askari wa kawaida na wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Diwani huyo alisema kundi hilo linalofanya mauaji katika wilaya za Kibiti na Rufiji bado lipo na lina nguvu.

“Linaonyesha bado lina uwezo mkubwa wa kufanya mauaji na kutokomea kusikojulikana,” alisema.

Alisema kwa sasa Serikali inapaswa kuongeza nguvu zaidi ya wapelelezi ili kukomesha kikundi hicho ambacho hakijajulikana kinafanya hivyo kwa sababu zipi na wala kinakojificha.

Akizungumzia ujumbe huo, kamanda wa polisi wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuwasaka.

“Tutapambana nao tu,” alisema Kamanda Lyanga na kukata simu.
Chanzo: Mwananchi

Comments