
Sheikh Yussuf Mecca, kutoka Columbus, Ohio
Na Swahilivilla Washington
Waislamu wametakiwa kuendeleza Ucha Mungu na mema waliyokuwa wakiyafanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Waislamu wametakiwa kuendeleza Ucha Mungu na mema waliyokuwa wakiyafanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Wito huo ulitolewa jana na Sheikh Yussuf
Mecca alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za Iddi zilizoandaliwa na
Jumuiya ya Waislamu wa Tanzania wa Jiji la Washington na Vitongoji vyake
ijulikanayo kwa jina la TAMCO.
“Kwa vile mwezi wa Ramadhani umekwisha
isiwe yale yote mazuri tuliyokuwa tunayafanya ikawa ndiyo basi, na
tusubiri Ramadhani nyengine” alisema Sheikh Yussuf.
Aliendelea kusisitiza umuhimu wa
kujitahidi kumcha Mungu wakati wowote na kujitahidi katika kutenda mambo
mema na ibada ili kujiandaa na safari ya Akhera ambayo inanaweza
kumfikia mtu wakati wowote.
” Hakuna hata mmoja ambaye anajua ni
siku gani atafumba jicho na atakufa”, alisisitiza Mgeni huyo rasmi
kwenye shere hizo, huku akitilia nguvu hoja yake kwa Aya ya Qur’an
isemayo: “كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ” (Kila nafsi itaonja
mauti/kifo), akigogoteza kuwa hakuna mtu yoyote anayejua atakufa lini au
mahali gani.
Aliongeza kusema kuwa kurejea kwenye
maasi baada ya juhudi kubwa za ucha Mungu na ibada katika mwezi wa
Ramdhani ni sawa na kuiharibu kazi ya kiufundi liyofumwa kwa juhudi na
ustadi mkubwa.

Mwenyekiti wa TAMCO Bwana Ali Muhammed
Sherehe za Iddi za Waislamu wa Tanzania
katika Mji huo Mkuu wa Marekani, ni utamaduni ulioanza tangu mwaka 1998,
ambapo Waislamu waliona haja ya kuwa na mjumuiko wa pamoja katika Siku
Kuu, ikizingitwa kuwa Marekani si nchi ya Kiislamu na kwa hivyo hakuna
sherehe rasmi za Iddi, kama alivyoelezea Mwenyekiti wa TAMCO Bwana Ali
Muhammed:
“Wazee na vijana waliokuwepo hapa katika
miaka hiyo waliona kuna haja ya kuanzisha Umoja ambao utawasaidia
katika mambo yao ya Kidini, siyo tu kwenye sherehe za Iddi, bali pia
katika maswala mengine ya sherehe na misiba. Na baada ya chombo hicho
kuanzishwa ndipo ukaanza utaratibu wa kuandaa sherhe kama hizi za Iddi”.
Bwana Ali aliesema kuwa sherehe hizi
zinakuja baada ya Mfungo wa Ramadhani ambapo jumuiya yake hukodi ukumbi
maalum kwa ajili ya futari ya pamoja kwa wanachama wake na wageni
wengine waalikwa kila siku za Jumamosi na Jumapili katika mwezi huo
mtukufu.
Aliendelea kusema kuwa sherehe hizi za
Iddi hufanyika kwa awamu mbili, asubuhi na jioni: “Mwanzo tulikuwa
tunafanya tu sherehe za wakati wa jioni, lakini baadaye tukaona kuna
haja ya kukutana pamoja wakati wa asubuhi, kwa vile kuna watu baada ya
kutoka Msikitini huwa hawana pa kwenda, kwa hivyo tukaona ni vizuri
tuianzie asubuhi ili watu walitoka Msikitini waje hapa wapate chai ya
asubuhi na baadaye kurejea tena jioni na kwa hivyo kufanikisha furaha
kwa siku nzima ya Iddi”
Akizungumza na Swahilivilla, Mwenyekiti
huyo wa TAMCO alidokeza kuwa jumuiya yake imekuwa ikikutana kila baada
ya muda fulani ili kupanga mikakati ya kuiendeleza jumuiya hiyo kwa
kupitia kamati zake mbali mbali, jambo ambalo limepelekea ufanisi mkubwa
na kuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa jumuiya za Watanzia nchini
Marekani.
Kama ambavyo penye mafanikio hapakosi
changamoto, TAMCO nayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za hapa na
pale. Miongini mwao ni uchache wa watu wa kujitolea katika matayarisho
ya shughuli za jumuiya na uendeshaji wake kwa ujumla.
Kwa hivyo, kiongozi huyo wa TAMCO
amewatolea wito wanajumuiya hiyo kujitokeza kwa wingi katika kujitolea
kwenye maandalizi ya shughuli zake na uendeshaji wake kwa ujumla
akisema:
“Jumuiya hii ni yetu sote, na
tutaiendesha sisi wenyewe, hakuna mtu ambaye atatoka sehemu nyengine
kuja kutusaidia kuiendesha, kwa hivyo ni kuweka nia zetu na kuweka
umuhimu tukizingatia kuwa chombo hiki ni cha kwetu, basi tufanye
jitihada zaidi za kukitunza.
Aidha alikumbusha kuwa TAMCO ni jumuiya
inayoendeshwa kutoka na ada na michango ya wanachama wake, na kwamba ni
muhimu kwa wanachama kujitahidi katika kutekeza wajibu wao wa kutoa
michango yao kwa wakati.
“Inapofika wakati wa kutoa michango
tutoe michango, kwani tukifanya hivyo chombo chetu kitakwenda mbali
zaidi”. Alisistiza Kiranja wa TAMCO, Bwana ali Muhammed.
Sherehe za Iddi za Wasialamu wa Tanzania
jijini Washington ni fursa nzuri kwa familia za wanachama wake ambapo
hutoa fursa kwa watoto kupata muda na sehemu ya kusherehekea na
kujisikia kuwa wako katika Siku Kuu wakiwa Ughaibuni.

Wa kwanza (kulia) Aziza Mattaka, Miriam Manu kutoka watatu (kulia) na rafiki zao
Miongoni mwa watoto waliopata nafasi ya
kuhudhuria sherehe hizo ni Miriam Manu, amabaye ameiambia Swahillivilla
kuwa anajisikia furaha kukamilisha funga ya Ramadhani na kuweza
kusherekea siku hii adhimu kwa Waislamu.
“Najisikia furaha na namshukuru Allah
kwa kila kitu alichoniwezesha kuwa nacho, khususan kuniwezesha kufunga
na kunifikisha katika siku hii na kusherehekea”, alisema msichana huyo
ambaye makazi ya ugenini yamemfanya asiweze kuzungumza Kiswahili, na
hivyo kuongea nasi kwa Kimombo.
Aliendelea kusema: “Mama yangu alikuwa
akiniambia kuwa kufunga kunakufanya ufahamu ni jinsi gani watu masikini
na waiokuwa na uwezo wanajihisi wanapokuwa na njaa, na hii inakupa moyo
wa kuwasidia watu wengine wenye matatizo na mambo kama hayo”
Miriam aliendelea kusema “Hii ni siku ya
furaha, kwani sote tunajumuika pamoja, tunaswali pamoja, tunacheza,
kucheka na kula pamoja. Ni siku ya furaha kwani tunapata nafasi ya
kukutana na marafiki wa zamani na kupata marafiki wapya, na ni jambo la
kusikitisha pale sherehe zinapomalizika tunalazimika kuagana na marafiki
zetu.
Itafaa kukumbusha kuwa Sherehe za TAMCO
huchukua masaa kadhaa, na kwa hivyo Waislamu hupata fursa ya kuswali
Swala za Alasiri, Mgharibi na Isha kwa jamaa katika viwanja hivyo, kama
alivyodokeza Miriam.
Naye msichana Sheri Juma hakusita kuelezea furaha yake kwa siku hii yenye umuhimu mkubwa kwa Waislamu.
“Siku ya Iddi ni siku ya furaha kwangu,
kwani huamka asubuhi kuonana na familia yangu, kisha tunakwenda kuswali
na kumshukuru Mola kwa kila alichonijaalia maishani mwangu, kisha
tunakuja hapa kukutana na marafiki”. Alisema Sheri kwa sauti na uso
wenye bashasha, huku midomo ikiwa tayari kuitafuna mishikaki.
Itakumbukwa kuwa nchini Marekani
kumekuweko na matukio ya hapa na pale yenye chuki dhidi ya Waislamu, na
kwa hivyo mikusanyiko kama hii ni nafasi ya kuimarisha mshikamano
miongoni mwa Waislamu kama anavyotukumbusha msichana Aziza Mattaka:
“Ni jambo la faraja kwetu kukutana
katika mjumuiko kama huu kama Jamii ya Waislamu khususan baada ya
matukio ambayo yamekuwa yakitokea katika siku za hivi karibuni yenye
kuonesha chuki dhidi ya Waislamu, kwa hivyo ni jambo la busara kukutana
kama hivi baada ya Mfungo wa Ramdhani, na najisikia faraja baada ya
kukamilisha Swaumu yangu na kuja kujumuika na jamaa na marafiki”.
Comments
Post a Comment