RC TABORA AWATAKA WADAU KUSAIDIA KILIMO CHA TUMBAKU KISISABABISHE JANGWA

Related image
Na Tiganya Vincent-RS-Tabora

WADAU wa zao la tumbaku  kutoka Tabora na Katavi wametakiwa kusaidia wakulima wa zao hilo kuendelea na kilimo hicho bila kuharibu mistu iliyopo kwa ajili ya kuyaepusha maeneo hayo kuwa katika tishio la kuwa jangwa.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri wakati akifungua mkutano wa siku wa wadau kutoka mikoa ya Tabora na Katavi.

Madhumuni ya mkutano huo ilikuwa ni kujadiliana ili kuja ya mpango wa kumsaidia mkulima wa tumbaku kuendelea na kilimo hicho huku akiwa na mipango endelevu ya utunzaji wa mistu.

Alisema kuwa mipango hiyo ni pamoja na kila mkulima kuwa na takwimu sahihi ya kuni zinazohitajika kwa mwaka katika ukaushaji wa zao lao ili ziendane na mipango ya upandaji wa miti mipya kwa wakulima hao katika maeneo yao.

Bw. Mwanri aliongeza kuwa mipango mingine ni pamoja na kuwaelimisha juu ya ujenzi wa majiko ya kisasa ya ukaushaji wa tumbaku ambayo mkulima anatumia matawi ya miti badala ya magogo ambacho ndio chanzo kikuu cha uharibifu wa mistu.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga alisema kuwa wakulima wa tumbaku katika eneo lake wamejitahidi kutumia majiko ya kisasa ambayo kwa kiasi kikubwa yamezuia ukataji ovyo wa mistu.

Alisema kuwa tatizo kubwa linalowakabili wao ni uvamizi wa makundi makubwa ya mifugo kutoka mikoa jirani ambapo inakadiriwa kuwepo na zaidi ya ng’ombe milioni 3 na hivyo kuvamia maeneo mbalimbali ya mistu na hifadhi.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Katavi alisema katika kukabiliana na tatizo hilo tayari wameshaondoa zaidi ya ng’ombe elfu 40 walikuwa wamevamia katika maeneo ya wilaya ya Tanganyika.

Meja Jenereali Mstaafu Muhuga aliongeza kuwa zoezi hilo la kuyaondoa makundi ya ng’ombe linatarajia kuendelea mwezi Julai mwaka huu.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tumbaku Tanzania Louis Roussos aliwaomba wadau kuwasaidia wakulima kuwa na mbinu mbadala ya kuendesha kilimo cha tumbaku kuwa kwa kuhakikisha kuwa mistu inakuwa endelevu.

Alisema kuwa kinyume cha hapo tumbaku ya Tanzania ipo hatarini kukataliwa na Kampuni kubwa duniani kwa sababu haziko tayari kununua zao ambalo linasababisha uharibifu wa mazingira.

Bw. Roussos aliongeza kuwa ni vema wadau wakatumia fursa hiyo kuhakikisha wanapata mikakati ya kuwasaidia wakulima wa tumbaku waendelee kunufaika na tumbaku huku wakitunza mistu.

Comments