Mawakili 248 waapishwa, Tundu Lissu awataka kutumia taaluma yao kusaidia jamii

 
Na Eliphace Marwa – Maelezo
 
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili wapya kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya uwakili na kutumia taaluma zao kwa kutoa msaada wa kisheria kwa jamii.

Aliyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa Sherehe za 56 ya kuwapokea na kuwaapisha Mawakili wapya 248 iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Aidha Kaimu Jaji Mkuu aliwahimiza Mawakili wapya kujiendeleza kitaaluma kwa sababu kuwa wakili sio mwisho wa taaluma kwani wanahitajika kusoma sheria za nchi mbalimbali Duniani ili kuweza kuingia mikataba ya kimataifa.

Alisema mawakili wapya wanatakiwa washiriki katika kutoa haki, wawe waaminifu kwa mahakama na wateja kwani wakienda kinyume haki itapotea.

“Mawakili wote wanatakiwa kuwa waaminifu kwa wateja wanaowahudumia na kushirikiana na mahakama katika kutoa haki na wasiwe mawakala wa rushwa bali wawe mawakala wa kutenda haki,” alisema Kaimu Jaji Mkuu Prof. Ibrahim.

Aidha Kaimu Jaji Mkuu aliwataka mawakili hao kufika maeneo ya nje ya mji ili wasaidie upatikanaji wa haki kwani kumekuwa na changamoto kubwa ya mawakili katika maeneo ya nje ya miji.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) Tundu Lissu aliwataka Mawakili hao kutumia taaluma hiyo katika kuisaidia jamii kujua haki zao na utawala wa sheria japo kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya sheria nchini.

“Napenda kuwatakia kila la kheri mawakili hawa wapya ila niwaombe watumie taaluma hii kwa kuisaidia jamii kujua haki zao pamoja na utawala wa sheria,” alisema Mh. Tundu Lissu.

 Idadi ya mawakili walioapishwa  jana imepelekea Tanzania kuwa na idadi ya zaidi ya mawakili 6300.

Comments