Kigamboni waomba KDA ivunjwe kama CDA

 Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile 
Na Hellen Mlacky
 
BARAZA Maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, limeiomba serikali kuivunja Mamlaka ya Uendelezaji Mji wa Kigamboni (KDA) na kukabidhi mpango wa uendelezaji wa mji huo na majukumu yote kwa Halmashauri ya Manispaa hiyo.

Ombi hilo lilitolewa katika mkutano maalumu wa Baraza hilo, uliolenga kujadili ajenda iliyoletwa na KDA kwa halmashauri kama Mamlaka ya Maamuzi ya Wananchi katika ngazi ya Manispaa na kuangalia kama kuna umuhimu wa kutekeleza kwa pamoja mpango huo au mamlaka mojawapo iweze kutekeleza majukumu ya mpango huo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile (pichani) alisema kwa sasa utekelezaji wa mpango huo, una mgongano mkubwa katika utendaji. Aliiomba serikali kukabidhi majukumu yote, yaliyokuwa yakifanywa na KDA kwa Halmashauri ya Manispaa hiyo ili kuyatekeleza na kuendeleza mji mpya wa Kigamboni.

“Tayari serikali imeonesha kwamba mnapokuwa na Mamlaka mbili za kusimamia jambo moja kama ilivyokuwa CDA na Halmashauri ya Manispaa Dodoma inaleta matatizo…Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni ni Mamlaka ambayo inaweza ikasimamia hili jambo, hivyo tunaiomba Serikali iivunje KDA na kukabidhi Mpango wa uendelezaji wa Mji wa Kigamboni kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni” alisema. Alisema, “eneo ambalo lipo kwenye mpango ni asilimia 12.7 ya ardhi yote ya Kigamboni na ni Kata sita kati ya Kata tisa ambazo zipo katika wilaya yetu ya Kigamboni, hivyo kwa ukubwa ni ndogo, ila kwa kata ni nyingi ambazo zinabeba uchumi wa wilaya na Halmashauri ya Kigamboni”.

Alisema, “KDA wamekuwa wanahodhi eneo kubwa la uendelezaji katika Kigamboni yetu, na kwa kuwa Rais ameshavunja Mamlaka ya CDA ambayo ina muundo na majukumu yanayofanana ya KDA, na kwa kuwa Halmashauri ya Kigamboni tupo vizuri na tupo imara kuweza kusimamia Kigamboni kwa ujumla wake, tumetoa mapendekezo ya kuomba serikali iivunje KDA na kukabidhi madaraka yake halmashauri”.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kigamboni, Maabadi Hoja alisema kuwa kazi zilizokuwa zikifanywa na KDA, sasa zimepata mfanyaji baada ya kuundwa Halmashauri ya Kigamboni, hivyo suala zima la upangaji mji limekabidhiwa Manispaa ya Kigamboni. “Sisi madiwani wote na watendaji wa Kigamboni sasa tunasema kazi hii ni ya Halmashauri na si ya KDA, Mamlaka hii inatosha, tunamuomba Rais aivunje KDA kama alivyoivunja CDA kwa sababu kuwepo mamlaka mbili sehemu moja taratibu lazima zisumbue na kutakuwepo na mgongano wa maslahi na ili halmashauri ikae vizuri lazima Mamlaka moja ife… Hivyo KDA ife ili sisi tuweze kufanya kazi,” alisema.

Alisema, “Tunaamini kwamba watendaji wa Kigamboni wanaweza kulifanya suala hili kwa umakini zaidi kwa kuwa KDA hawana watumishi wa kutosha n a wajumbe wote kwa wameridhia kwamba Mamlaka ya Manispaa ya Kigamboni ina haki zote za kufanya kazi hii ya kuijenga Manispaa ya Kigamboni badala ya KDA” . Alisema, “KDA haina rasilimali fedha na haina rasilimali watu hata ule mpango haujakamilika mpaka sasa, serikali imeanzisha halmashauri hii ni mamlaka iliyokamilika na inajitegemea”.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Stephen Katemba alisema madiwani wameamua kwa kauli moja wanataka KDA ivunjwe kwa sababu imeanza shughuli zake muda mrefu takribani miaka saba, lakini hadi sasa kilichotegemewa kufanyika hakijafanyika na hiyo inatokana na uhaba wa rasilimali.

“Nimeona mvutano baadhi ya mambo mbalimbali…Maamuzi ya wananchi ndiyo tutakayoyaidhinisha na kuyapeleka katika mamlaka husika ili maamuzi yaweze kufanyika kuona kama kuna umuhimu wa kuendelea kuwepo na KDA au la au Manispaa inatekeleza maamuzi katika utaratibu gani.

Manispaa ipo tayari kuona namna bora ya kuendeleza mji wa Kigamboni,” alisema. Alisema, “KDA wanategemea watumishi wa halmashauri wakiwemo watendaji wa kata na halmashauri ambao ndiyo wanawasaidia kutekeleza majukumu yao lakini wanaripoti kwa mwajiri wao ambao ni Serikali kupitia Manispaa hivyo lazima wapate utaratibu… tutaiachia mamlaka husika kujadili mapendekezo ya Madiwani na baadae waweze kutoa maamuzi”.

Juni 19, 2012 Serikali iliagiza eneo la Kigamboni liendelezwe kuwa Mji wa Kisasa na pia Mpango wa Uendelezaji eneo hilo, utekelezwe kwa awamu tatu kuanzia Julai 2012 hadi mwaka 2031 ambapo pia iliagiza kuundwa wakala wa kusimamia uandaaji na utekelezaji wa Mpango wa Uendelezaji Mji wa Kigamboni(KDA). Pamoja na hayo, lakini zimejitokeza changamoto katika mpango huo ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha za kutekeleza mpango huo, ambazo zaidi ya Sh trilioni 12 zilikadiriwa kuhitajika kwa ajili ya ujenzi wa mji.

Changamototo nyingine ni kuwepo mamlaka mbili ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni iliyoanzishwa Desemba 2015 na KDA zinazotekeleza majukumu yanayofanana katika eneo moja. Wakati wakitaka KDA ivunjwe, Mei 15 mwaka huu Rais Dk John Magufuli alivunja rasmi Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na kuagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA, zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

Rais Magufuli alisema aliamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi, uliokuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili na pia kuendana na mahitaji ya sasa, ambayo yalidhihirisha kuwa hakukuwa na haja ya kuwepo kwa CDA.

Comments