Mbunge kulipia dawa watoto, wajawazito wanaonyanyaswa


MBUNGE wa Jimbo la Kahama, Jumanne Kishimba, ameahidi kuwalipia watoto chini ya miaka mitano, wazee wasiojiweza na wajawazito wanaokosa dawa wanapokwenda hospitalini wakati walitakiwa kupatiwa matibabu bure.
Kishimba alitoa ahadi hiyo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Wendele katika mkutano wa hadhara, ambako alisema makundi hayo ambayo yanatibiwa bure yamekuwa yakinyanyapaliwa huku wakiambiwa kuwa hakuna dawa pindi wanapoenda hospitali kupatiwa matibabu. Alisema tatizo hilo la kukosa dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama limekuwa kubwa hasa kwa makundi hayo yasiyojiweza hali ambayo wakienda kupatiwa matibabu wamekuwa wakiambiwa kwenda kununua dawa katika maduka yaliyopo jirani na hospitali hiyo.
Aidha, mbunge huyo amewataka wananchi wa jimbo lake kutumia chakula walichonacho kwa uangalifu kwani mwaka huu kuna uwezekano wa kuwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na mwaka huu kuwa na upungufu wa mvua za masika. “Kwa sasa wananchi ni bora mkalima mazao yanayostahimili ukame kutokana na mvua za masika mwaka huu kuwa kidogo msiuze chakula kilichopo badala yake mkitumie vizuri ili kiweze kuwasaidia hadi msimu ujao wa mvua za masika,” alisema Kishimba.
Kuhusu umeme katika kata hiyo, Kishimba alisema mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu umefunguliwa na kata hiyo ipo kwenye mpango wa kupata nishati hiyo na kuwataka wananchi hao kuwa wavumilivu kwani kufikia mwaka 2019 tatizo hilo litakuwa limekamilika. “Niwambie wananchi suala la umeme kata yenu ipo kwenye mpango wa kupatiwa huduma hiyo kwa (REA) awamu ya tatu iliyofunguliwa hivyo kuweni wavumilivu hadi 2019 tatizo litakuwa limekwisha,” alibainisha Kishimba.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Wendele, Waitare Kishamuli, alimwambia mbunge huyo kuwa kwa mwaka huu mazao mengi yameungua na jua hali ambayo inatishia kuwepo kwa baa la njaa iwapo wananchi hao wasipopatiwa chakula kwa muda unaotakiwa ili kuwanusuru na hali hiyo

Comments