
Katika
kuhakikisha kuwa biashara haramu ya dawa za kulevya inakomeshwa hapa
nchini na kwa kuzingatia dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya
kupambana na tatizo la dawa za kulevya, Jeshi la Polisi nchini limetoa
maelekezo kwa Makamanda wa Polisi katika mikoa yote kuongeza nguvu za
Oparesheni katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya
kwa kuwakamata wanaotumia, wanaouza na wanaosafirisha.
Aidha,
Jeshi la Polisi nchini limewaagiza Makamanda wote pindi wanapoendesha
oparesheni dhidi ya dawa za kulevya kutokuangalia sura ya mtu, cheo,
wadhifa wala nafasi aliyonayo katika jamii.
Katika
hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini linakemea vikali tabia ya baadhi
ya wananchi wanaokusanyika katika vituo vya Polisi pindi baadhi ya
watuhumiwa wa makosa mbalimbali wanapotakiwa kufika kwenye vituo hivyo
kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma wanazokabiliwa nazo. Ni
marufuku kwa mtu ama kikundi chochote kukusanyika katika kituo cha
Polisi bila ya kuwa na sababu ya msingi na watakaobainika
watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Jeshi la
Polisi nchini, linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za
uhalifu na wahalifu zikiwemo za watu wanaojihusisha na biashara haramu
ya dawa za kulevya na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa siri ili
kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya usalama.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba-ACP,
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
MAKAO MAKUU YA POLISI.
Comments
Post a Comment