Baada
ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza watumishi wote wa Manispaa ya Bukoba
mkoani Kagera waliohusika katika ukarabati wa majengo ya Shule ya
Sekondari Omumwani ambayo yameonekana kutoendana na thamani ya fedha
zilizotumika wachunguzwe, watumishi watatu wa manispaa hiyo
wamesimamishwa kazi.
Watumishi
hao walisimamishwa jana na Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Diwani
Athumani, baada ya kufanya ukaguzi wa miundombinu ya maji iliyomo katika
majengo ya shule hiyo.Shule hiyo ilikarabatiwa kuwapa hifadhi ya muda
wanafunzi wa shule za sekondari Ihungo na Nyakato zilizoathiriwa na
tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, Septemba 10, mwaka jana.
Baada
ya ukaguzi huo, Athumani alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya
Bukoba, Chibunu Lukiko, kumtajia majina ya watumishi waliohusika moja
kwa moja katika usimamizi wa kila siku wa shughuli hiyo.
Katika
maelezo yake, Athuman alisema aligundua ukarabati uliofanywa ulikuwa
chini ya kiwango na hauendani na thamani ya Sh milioni 119 zilizotolewa
na Serikali.
“Kwanini
wakurugenzi hampendi kufuatilia miradi iliyo katika maeneo yenu? Kama
mngefuatilia mapema, mngegundua ubadhilifu uliofanyika hapa na kuchukua
hatua mapema.
“Kwa
hiyo, naagiza kuanzia leo Januari 3 (jana), mkurugenzi wa Manispaa ya
Bukoba uwasimamishe watumishi wote waliohusika ambao ni Mhandisi Kitengo
cha Ujenzi wa Manispaa ya Bukoba, Andondile Mwakitalu, Mhandisi
Msaidizi, Costane Felix na fundi Charles Kafumu.
“Hawa
lazima wasimamishwe ili kupisha uchunguzi utakaofanyika kwa ajili ya
kulinganisha kazi iliyofanywa na kiasi cha fedha kilichotumika kama
vinaendana.
“Tatizo
jingine nililoligundua ni kutokuwapo kwa usimamizi mzuri wa mradi huo
kutoka kwa watumishi wa manispaa. Hao nao uchunguzi dhidi yao utafanyika
kwa uwazi na ukweli na hatutamwonea mtu.
“Sitaki kusikia shughuli hii inasimama eti kwa sababu ya hawa watu wamesimamishwa, fanya makabidhiano na wale watakaokuwapo.
“Kaimu
mkurugenzi hakikisha mnakabidhiana kila kitu, hata msumari usibaki na
uchague watu wengine wa kuendelea na kazi ya kusimamia mradi huu ili
ukamilike kwa muda uliopangwa,” alisema.
Naye
Mhandisi Mwakitalu aliyesimamishwa, alisema majengo hayo yalikuwa
katika hali mbaya na kwamba ukarabati wake unahitaji fedha nyingi ili
yarudi katika hali yake ya kawaida.
Comments
Post a Comment