Maofisa
watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wanaotuhumiwa
kushiriki kumwondoa faru John kutoka katika Creta hiyo walikamatwa juzi
kwa mahojiano ili kujua ukweli kuhusu mazingira ya kupotea kwake.
Hatua
ya maofisa hao kukamatwa imekuja siku tatu baada ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa kuituhumu menejimenti, wafanyakazi wa NCAA na Baraza la
Wafugaji (NPC) kuwa imejaa vitendo vya rushwa na wizi na asingeweza
kuvumilia sakata la faru John ambaye alisema kuwa aliuzwa kwa Sh200
milioni kwenye Hoteli ya Grumet iliyo Hifadhi ya Serengeti na kuwa
walipokea fedha za awali Sh100 milioni.
Waziri
Mkuu alisema anataka kumwona faru huyo, nyaraka za kumhamisha na kama
amekufa basi apelekewe hata pembe ofisini kwa kuwa anajua pa
kuzipeleka.
Alisisitiza kuwa ikibainika kuna ambao wamekiuka taratibu watawajibika.
Habari
za uhakika kutoka Ngorongoro, ambazo zimethibitishwa na Jeshi la Polisi
zinasema kuwa maofisa hao watano wanashikiliwa katika kituo chao cha
Ngorongoro kutokana na ushiriki wao kwa njia moja au nyingine.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Israel Naman ambaye alikuwa Kaimu mkuu wa idara ya uhifadhi wakati faru huyo akiondolewa.
Wengine
ni Cuthbert Lemanya, ambaye alikuwa Mkuu wa Kanda ya Creta, Dk Athanas
Nyaki ambaye anadaiwa kumdunga sindano ya usingizi ili aweze kubebwa.
Maofisa
wengine waliokamatwa ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii
wa Mamlaka ya Ngorongoro, Kuya Sayaleli na aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Idara
ya Ikolojia, Patrice Mattey.
Ofisa
mmoja wa NCAA, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake jana alisema
maofisa hao walikamatwa juzi jioni na jana walikuwa wanaendelea
kuhojiwa.
“Tuiache serikali ifanye kazi kwani ni muhimu sana kujulikana ukweli wa tukio hili,” alisema ofisa huyo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo hakupatikana jana kuelezea
tukio la kukamatwa maofisa hao, baada ya simu yake kupokelewa na
msaidizi wake ambaye alieleza yupo kwenye kikao.
Lakini,
ofisa wa mmoja wa polisi, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina kwa kuwa si
msemaji alikiri kukamatwa maofisa hao kwa mahojiano.
Chanzo cha sakata
Akiwa
katika ziara ya kikazi Ngorongoro, Waziri Majaliwa aliibua sakata la
kuhamishwa kinyemela faru huyo na kudaiwa kupelekwa Grumet.
Waziri
mkuu alitaka ukweli kuhusu upotevu wa John aliyeondolewa Creta na
kupelekwa Grumet na kudaiwa kufa huku taarifa za kifo hicho zikifanywa
siri.
Waziri Mkuu alitaka kupewa nyaraka zote zilizotumika kujadili kumuondoa faru na kuamua kumpeleka Grumet.
Comments
Post a Comment