Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt.Medard Kalemani, akizungumza jambo wakati wa Mkutano wake na
wananchi wa Kijiji cha Kishuro,Kata ya Ngenge Wilaya ya Muleba, Mkoa wa
Kagera. Dkt.Kalemani amefanya ziara Wilayani humo ya kukagua Mradi
utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili na kueleza mipango ya Serikali
kutekeleza Awamu ya Tatu ya mradi husika.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt.Medard Kalemani, akizungumza jambo wakati wa Mkutano wake na
wananchi wa Kata ya Ngwanseri,wilaya ya Muleba, wakati wa ziara yake ya
kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi
Richard Ruyango,akizungumza jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalema ni kukagua utekelezaji wa Mradi wa
REA Awamu ya Pili.Wengine katika picha ni baadhi ya Viongozi wa
Halmashauri hiyo,Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini,
REA,TANESCO, na Wakandarasi wanaotekeleza mradi husika.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt.Medard Kalemani, (Wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na Mbunge
wa Jimbo la Muleba Kusini, Prof.Anna Tibaijuka (wa pili kushoto),Mkuu
wa wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Ruyango,(wan ne kushoto)pmoja na
Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, REA,TANESCO, na Wakandarasi
wanaotekeleza mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mmoja wa Wananchi katika akiuliza jambo
wakati wa mkutano wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard
Kalemani(hayupo pichani) katika Kata ya Ngwanseri.
Wananchi wa Kata za Ngwanseri na Ngenge
wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt.Medard Kalemani na
ujumbe wake wakati wa ziara yake a kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA
Awamu ya Pili wilayani Muleba.
Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini
Prof.Anna Tibaijuka (kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini,Dkt.Medard Kalemani ( katikati) mara baada ya kumaliza mkutano
wake na wananchi wa Kijiji cha Kishuro. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya
Muleba Mhandisi Richard Ruyango.
Wananchi
wa Kijiji cha Kishuro Wilaya ya Muleba, wakisoma Jarida la Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), wakati wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na
Madini,Dkt.Medard Kalemani (hayupo pichani) akieleza utekelezaji wa
Mradi wa REA Awamu ya Pili na mipango ya Serikali ya kutekelza REA Awamu
ya Tatu.
Na Asteria Muhozya, Muleba
Imeelezwa
kuwa, Serikali imepanga kutumia Nguzo za Zege katika utekelezaji wa
Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaotarajia kuanza
kutekelezwa kuanzia mwezi Januari, 2017 chini ya Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Hayo
yamebainishwa kwa nyakati tofauti na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt. Medard Kalemani wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa
mradi wa REA Awamu ya Pili katika Kata za Ngenge na Ngwanseri, Wilayani
Muleba Mkoani Kagera, pamoja na kueleza mipango ya Serikali katika
utekelezaji wa mradi husika Awamu ya Tatu.
Dkt.
Kalemani amesema kuwa, lengo la kutumia nguzo hizo za zege ni kutokana
na uimara wake utakaowezesha upatikanaji umeme wa uhakika na kuepuka
kuchomwa na kuongeza kuwa, tayari nguzo hizo zimeanza kutumika katika
Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumzia
utekelezaji wa REA Awamu ya Pili, amesema Serikali imetekeleza mradi
huo kwa kasi kubwa kutokana na dhamira yake ya kuhakikisha kuwa,
ifikapo mwaka 2025 asilimia 75 ya Watanzania wawe wameunganishwa na
nishati hiyo ambayo ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi.
“ REA
awamu ya pili imekamilika kwa kiwango kikubwa. Vipo baadhi ya vijiji
havijafikiwa kutokana na dosari ndogo ndogo lakini tutavikamilisha
kuwezesha utekelezaji wa Awamu ya Tatu. Hata katika Wilaya hii vipo na
tayari nimemwelekeza Mkandarasi kukamilisha kazi hiyo
haraka,”amesisitiza Dkt. Kalemani.
Akielezea
mipango kwa Awamu ya Tatu, amesema kuwa, Serikali imelenga kuhakikisha
kuwa, awamu hiyo inavifikia vijiji vyote ambavyo havikuunganishwa katika
Awamu ya Pili, visiwa vyote, Taasisi mbalimbali, Sehemu zinazotoa
Huduma za Kijamii zikiwemo za Afya, shule na visima vya maji.
Aidha,
alisema kuwa, kukamilika kwa utekelezaji wa Miradi Ujenzi wa njia za
Kusafirisha umeme wa Msongo Mkubwa wa kV 400 kutoka Iringa hadi
Shinyanga kupitia Dodoma na Singida kutawezesha upatikanaji wa umeme wa
uhakika pamoja na kuchochea uchumi wa viwanda hususan katika mikoa ya
Kanda ya Ziwa.
Wakati
huo huo, Dkt. Kalemani ametumia fursa hiyo kuzitaka Halmashauri zote
nchini kushirikiana na TANESCO kuweka utaratibu shirikishi ambao
utawawezesha wananchi kupata huduma za kuunganishiwa nishati hiyo
kupitia utaratibu wa kuanzisha madawati ya TANESCO katika maeneo
yatakayotambuliwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa
urahisi.
“TANESCO
na Halmashauri, pangeni namna ya kuwawezesha wananchi kufikiwa kwa
urahisi na huduma za kunganishwa nishati ya umeme. Mkubaliane kupanga
siku maalum ambayo wananchi watahudumiwa. Serikali inataka kila
mwananchi apate umeme, hivyo tuweke utaratibu ambao utarahisisha na
kuwezesha azma hiyo kufikiwa kwa haraka,” amesisitiza Dkt. Kalemani.
Pia, Dkt.
Kalemani amewataka Wakandarasi wote wakati wa utekelezaji wa miradi ya
Awamu ya Tatu kuhakikisha kuwa, wanajitambulisha katika Halmashauri na
Mamlaka nyingine ili waweze kutambulika ili kuepusha udanganyifu.
Vilevile,
Dkt. Kalemani ameitaka TANESCO kuwaidhinisha Wakandarasi wote
watakaofanya kazi ya ‘wiring’ katika nyumba za wananchi katika
utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu ikiwemo kutoa orodha zao ili
kuwapunguzia wananchi kero ikiwemo kuwaepusha na utapeli unaofanywa na
baadhi ya wasiowaaminifu.
Akizungumzia
Sekta ya Madini, Dkt. Kalemani amewahamasisha wachimbaji wadogo wadogo
kujiunga katika vikundi ikiwemo kujisajiri katika Ofisi za Madini
zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwawezesha
wachimbaji hao kuomba ruzuku kupitia vikundi pindi zinapotolewa na
Serikali.
Katika
ziara ya kutembelea Kata hizo, Dkt. Kalemani ameambatana na Mkuu wa
Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyango, Wataalam kutoka Wizara ya
Nishati na Madini, REA, TANESCO na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa
REA Awamu ya Pili Wilayani humo.(P.T)
Comments
Post a Comment