WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wadau wa elimu mkoa wa Mbeya kujitafakari baada ya Mkoa huo kufanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa darasa saba mwaka huu.
Profesa Ndalichako ametoa agizo hilo kwenye Mahafali ya Pili ya Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi Elimu ya Chuo cha Wakala wa Maendeleo ya Utawala wa Elimu(ADEM) yaliyofanyika jijini Mbeya.
Amesema  mkoa wa Mbeya umekuwa wa 22 kati ya mikoa 26 hivyo kudhihirisha kuwa ulifanya vibaya na ni lazima kila mdau ajitafakari ni kwa namna gani amechangia matokeo hayo mabaya.
Ameagiza uongozi ngazi ya mkoa na halmashauri kuhakikisha unajipanga kutumia fursa zilizopo ili kuondokana na aibu kwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa.
Amewataka pia walimu wakuu kuhakikisha wanakuwa wasimamizi wa kwanza wa raslimali za shule sambamba na kusimamia viwango bora vya taaluma.
Wahitimu wa mafunzo hayo ya mwaka mmoja ambao wote ni walimu wakuu kutoka shule za mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Iringa, waliiomba Serikali kuendeleza kozi hiyo wakisema imewajengea uwezo zaidi wa kiutawala.
Mwalimu Josephat Mahimbi akisoma risala alisema, awali walimu wakuu walikuwa na wakati mgumu kiutendaji kwa kuwa walikuwa wakiteuliwa kushika nyadhifa hizo pasipo kuwa na muongozo wowote

Comments