Watoto wenye kisukari wataka bima ya afya


SERIKALI na wadau wameombwa kutambua uwepo wa watoto wenye kisukari hapa nchini na kuweka mipango endelevu ya upatikanaji wa huduma za afya na jamii ikiwamo ya kuwakatia bima ya afya.
Ombi hilo limetolewa na Anita Bulindi wakati wa kusoma risala ya watoto wenye kisukari baada ya kukamilika kwa matembezi ya kuadhimisha Siku ya Kisukari Duniani.
Alisema watoto wenye kisukari wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika huduma za afya na kijamii ambazo zinaweza kutatuliwa kwa kuweka mipango endelevu ya upatikanaji wa huduma za afya.
Bulindi alisema gharama kubwa ya matibabu imekuwa changamoto kubwa kwa watoto na hii imetokana na kutokuwa na bima ya afya huku asilimia 17 ya watoto wenye kisukari ambao ni zaidi ya 1,900 ndio wenye kadi za Bima ya Afya.
“Tunaomba bima za Afya ili tuweze kupata matibabu bora, kubwa zaidi tungeomba matibabu au sawa za kisukari zitolewe bure kama ilivyo kwa wagonjwa wa HIV na wale wanaotumia dawa za kulevya,” alisema.
Mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, Mama Salma Kikwete ambaye ni mlezi wa Chama cha Watoto wenye Kisukari Tanzania (TDYA) aliwataka watoto na vijana wenye ugonjwa huo kutunza afya zao kwa kuwa na nidhamu katika matumizi ya chakula.
Mama Salma ndiye aliyeongoza matembezi ya zaidi ya kilometa mbili kutoka fukwe za Bahari ya Hindi eneo la Aga Khan hadi viwanja vya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDYA), Ramadhan Mongi alisema ili kukabiliana na changamoto ya vijana wenye ugonjwa huo kuwezeshwa ili wajigharamie, wameanzisha mfuko ambao unatoa mikopo kwa vijana ili waweze kufanya shughuli za kujiingizia kipato kitakachowasaidia gharama za matibabu.
“Mfumo ndio umeanza na hauna rasilimali za kutosha, tulianzisha baada ya vijana wakifikisha miaka 18 wanaonekana ni watu wazima huku hawana uwezo wa kumudu gharama,” alisema.

Comments