Na Jacquiline Mrisho, Dodoma.
Serikali
imetenga jumla ya shilingi bilioni 13.17 katika Bajeti ya mwaka
2016/2017 kwa lengo la kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya mkoa
wa Ruvuma ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata maji safi na
salama.
Kiasi
hicho cha fedha kimetajwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge alipokuwa akijibu swali la Mhe.
Jacqueline Ngonyani (Viti Maalum) lililohoji juu ya muda ambao Serikali
itapeleka majisafi na salama katika Mkoa huo.
Waziri
amesema kuwa Mpango wa Utekelezaji wa Maji Vijijini ulioanza mwaka
2006/ 2007, mkoa wa Ruvuma ulipangiwa vijiji 80 na kati ya vijiji hivyo
jumla ya vijiji 76 vilipata maji safi na salama.
“Asilimia
kubwa ya vijiji vilivyokuwa katika miradi hiyo vimepata maji safi na
miradi iliyobakia ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji hivyo kwa
mwaka huu wa fedha Ruvuma imetengewa kiasi cha fedha cha bilioni 13.17
ili changamoto ya maji safi na salama katika mkoa huo iishe kabisa”,
alisema Lwenge.
Ameongeza
kuwa Serikali imeendelea na mipango ya kuboresha huduma hizo katika
miji ya Songea, Mbinga, Namtumbo na Tunduru iliyopo katika mkoa huo
ambapo kwa mji wa Songea, mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji cha mto
Ruhila Darajani umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6.
Amefafanua
kuwa kukamilika kwa chanzo hicho mnamo mwezi Februari mwaka huu
kumeongeza kiasi cha upatikanaji wa maji wa jumla ya lita milioni 6 kwa
siku ambapo wakazi 164,162 wamenufaika katika Manispaa hiyo.Aidha,
Mhandisi Lwenge amebainisha kuwa kwa sasa Serikali imekamilisha usanifu
wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya uboreshaji wa
huduma hizo katika miji iliyopo katika mkoa huo.
“Serikali
inaendelea na jitihada ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi hiyo ambayo kwa mji wa Tunduru mradi utagharimu Dola za
Kimarekani milioni 7.3, mji wa Namtumbo ni Dola za Kimarekani 12.08, na
Dola za Kimarekani 11.86 kwa ajili ya mji wa Mbinga”, alisema Mhandisi
Lwenge.
Comments
Post a Comment