Waziri, mawaziri matatani kwa kutumia WhatsApp


Malcolm Turnbull, Waziri Mkuu wa Australia
SYDNEY, AUSTRALIA

WAZIRI Mkuu wa Australia, Malcolm Turnbull, ameingia katika mzozo na wataalamu wa usalama nchini humo kutokana na tabia yake ya kutumia mtandao wa WhatsApp kuendesha mijadala nyeti kitaifa, kati yake na mawaziri, pamoja na maofisa wengine waandamizi.

Mtandao wa WhatsApp nchini humo haujaunganishwa katika mfumo maalumu wa kitaifa kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za mijadala au mawasiliano rasmi ya viongozi.

Kutokana na hali hiyo wataalamu wa usalama wameonya wakisema ni hatari kwa usalama wa taifa lao.
Maofisa hao waliomo katika kundi moja la WhatsApp linalomjumuisha waziri mkuu na mawaziri wengine waandamizi ni pamoja na wanadhimu mbalimbali serikalini, washauri wa masuala ya habari katika ngazi ya wizara, wachumi waandamizi, wabunge na baadhi ya watumishi wa bunge.

Takriban maofisa wanne waandamizi wa usalama nchini humo wameweka bayana maoni yao kuhusu mwenendo huo wa waziri mkuu Turnbull na serikali yake kwenye matumizi ya WhatsApp.
Craig Searle, mwasisi wa taasisi ya ushauri kuhusu masuala ya usalama inayoitwa Hivint, ameweka bayana kwamba mfumo wa mawasiliano wa WhatsApp unaweza kutumiwa na viongozi katika masuala yasiyohusisha taarifa za serikali na ikiwa kinyume cha hapo ni hatari.

"Watumishi wa serikali wanapaswa kuwa makini zaidi kuhusu namna wanavyojadili taarifa za siri mitandaoni. Kwa kweli wanatakiwa kutumia mifumo salama na ambayo imeidhinishwa na inaratibiwa na Serikali ya Australia," alisema na kusisitiza kwamba mtandao wa WhatsApp haumo katika orodha ya mitandao iliyoidhinishwa kwa viwango vya usalama nchini Australia.

"…kama mwajiriwa wa serikali atahamisha taarifa za siri kupitia mtandao ambao haujaunganishwa katika ‘seva’ ya serikali ni lazima atakuwa anafanya kitendo cha kuhatarisha usalama wa nchi," alisema
Mtandao wa WhatsApp unatajwa kuwa na watumiaji takriban bilioni moja ambao kupitia mtandao huo hupata fursa ya kutumiana ujumbe kwa maandishi kati ya mtu na mtu au muunganiko wa watu kadhaa katika makundi, kutumiana video au sauti na zaidi ya hapo, kupigiana simu. Ni mtandao unaomilikiwa na mtandao mwingine wa Facebook.

Msemaji wa Serikali ya Australia amesema makundi ya WhatsApp yameundwa na kutumika ili kurahisisha mawasiliano na uratibu wa masuala kadhaa miongoni mwa watumishi wa serikali, ingawa pia hakuthibitisha kuwapo kwa kundi la WhatsApp la mawaziri, akisisitiza kuwa taarifa nyeti za serikali zimekuwa zikidhibitiwa na kwamba serikali imeweka itifaki maalumu juu ya matumizi ya simu au vifaa vingine vya mawasiliano.
Mtaalamu wa masuala ya usalama katika mitandao kutoka Taasisi ya Australian Strategic Policy, Tobias Feakin, anasema licha ya kuwapo kwa usalama wa kiwango fulani wa ujumbe unaotumwa kupitia WhatsApp lakini bado umakini unahitajika zaidi
.
"Hatari iliyopo katika WhatsApp, licha ya usalama wa kimawasiliano, ujumbe unaotumwa na mtu au watu fulani unakuwa katika mzunguko, sasa swali la kutafakari ni je, ujumbe huo unamfikia mtu wa mwisho akiwa na nia gani?" anasema Dk. Feakin

Waziri Mkuu Turnbull amekuwa akijulikana kuwa kipenzi cha matumizi ya vifaa vipya kiteknolojia kama saa aina ya Apple na mawasiliano kwa njia mbalimbali za kiteknolojia hasa mitandao ya WhatsApp na Wickr.
Inaelezwa kwamba mapema baada ya kupata wadhifa wa waziri mkuu alipendekeza mawaziri wake watumie zaidi mtandao katika mawasiliano au mijadala inayohusiana na kazi.

Ofisa mmoja wa ngazi za juu amekaririwa akisema waziri mkuu huyo amekuwa akipenda sana kutumia WhatsApp na kwa sababu hiyo, mawaziri wengine wamelazimika kuiga mwenendo wake huo.
Hali hiyo inajitokeza nchini Australia katika wakati ambao nchini Marekani, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic, Hillary Clinton, akikabiliwa na lawama za kufanya mawasiliano ya kiofisi kwa kutumia mfumo wa anuani binafsi za barua pepe badala ya ule rasmi kitaifa.

Wasiwasi bado umejikita kwa wataalamu wa usalama nchini Australia hasa hayo matumizi ya WhatsApp ikidaiwa kwamba maandishi ya kwenye mtandao huo hayaingii katika ‘seva’ ya serikali.
Katika hatua nyingine, hasa baada ya kutokea hali hiyo ya wasiwasi, wamejitokeza mawaziri wanaomtetea waziri mkuu wao.

Dan Tehan, anasema; "Kile ninachoweza kusema ni kwamba serikali, mawaziri, wabunge wawe makini."
Kwa upande wao mawaziri Steve Ciobo na Anne Ruston wanakiri kutumia mitandao hiyo isiyoungishwa katika ‘seva’ ya serikali, wakisisitiza kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kwa kuendesha mijadala isiyohusu mambo nyeti ya ofisi.
Raia Mwema

Comments