SERIKALI imedhamiria kuwekeza na kutekeleza sera na mipango ya kupunguza tatizo la maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na vifo vya uzazi hususani kwa vijana wa kike ambao ndio wamebainika kuwa sehemu kubwa ya watu wanaopata maambukizi ya ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangallah, watu wazima wamekuwa na mtindo wa kuanzisha uhusiano na mabinti wadogo, hali inayochangia vijana hao kuusambaza ugonjwa huo kwa vijana wenzao, hivyo kuongeza kasi ya maambukizi.
Dk Kigwangallah aliyasema hayo mjini Dodoma juzi wakati akizungumza kwenye semina ya siku mbili ya wabunge kuhusu matatizo ya maambukizi ya Ukimwi, vifo vya uzazi na mimba za utotoni iliyoandaliwa na Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids).
Alisema kwa tathmini iliyofanywa imebainika kuwa watu wazima wengi ambao tayari wana wenza wao, hupenda kuanzisha uhusiano na vibinti vidogo ambao nao wana wenza wao na matokeo yake ugonjwa huo husambazwa kwa kasi kupitia mzunguko huo.
“Tafiti zinaonesha kuwa vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 19 wanaoshiriki kwenye vitendo vya ngono wanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka, ingawa asilimia 40 kwa upande wa vijana wa kike na asilimia 47 ya vijana wa kiume tayari wana ufahamu wa tatizo la ugonjwa huo wa Ukimwi,” alisisitiza.
Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, alisema ni jukumu la wabunge kutumia fursa na wajibu wao wa kuishauri na kusimamia serikali na kuhakikisha inatekeleza mipango na mikakati yake iliyojiwekea katika kushughulikia matatizo hayo ya maambukizi ya Ukimwi, vifo vya uzazi na mimba za utotoni.
Mkurugenzi wa Miradi na Mshauri wa Sera za Masuala ya Ukimwi SADC, Boemo Sekgoma aliishauri serikali iangalie namna ya kutoa kipaumbele katika masuala ya afya ya uzazi wa mpango kutokana na ukweli kwamba takriban asilimia 80 ya bajeti ya masuala hayo inatoka nje ya nchi na wakati mwingine haitoki kwa wakati

Comments