OKTOBA
5, SIKU YA MWALIMU DUNIANI
Na, Doto Biteko
Leo
tarehe 5/10/2016 ni siku ya MWALIMU DUNIANI.
Katika nchi nyingi duniani ni siku ambayo pia
watu hutambua kazi za waalimu na hutumika kuwapa heshima kwa kutambua mchango
wa MWALIMU katika Jamii. kila nchi huwa na namna yake ya kuadhimisha siku hii
muhimu mfano katika nchi ya Afghanistan siku hii shule zote hufungwa na walimu
na wanafunzi pamoja hukusanyika kwenye shule husika huaandaliwa chakula cha
asili, muziki wa asili na burudani mbalimbali kwa ajili ya walimu na badaye
zawadi mbalimbali hutolewa kwa walimu.
Kwa
kifupi huwa ni siku ya furaha sana kwa walimu maana huinua hali ya kufanya kazi
na huwavuta watoto wengi kuipenda kazi ya ualimu.
Siku
ya leo imenipa tafakari sana, nimekumbuka nilipoanza Safari ya kuuelekea ualimu
pale chuo cha ualimu Katoke ilikuwa safari iliyojaa furaha na matumaini mengi
nakumbuka nilipofika getini kulikuwa na walinzi (wanachuo) wakanikaribisha karibu
sana Mwalimu nilianza kujiuliza hivi tayari nimekua mwalimu? Furaha
yangu ilizidi sana. Baada ya kumaliza masomo ya ualimu niliajiriwa kama mwalimu
daraja la IIIA katika shule ya msingi Nyang’hanga, niliianza kazi hiyo kwa
mapenzi yangu yote!
Niliipenda
kazi yangu, niliyapenda mazingira pamoja na kwamba ilikua kijijini sana(pengine kwasababu pia nilizaliwa na kukulia
kijijini sana) niliwapenda sana wanafunzi wangu. Nilijiona mwenye bahati
kuheshimika kama mzazi katika umri ule mdogo wa miaka23, jamii walinipenda na
wanafunzi wangu walinipenda sana.
Niliposhika
zamu yangu ya wiki wanafuzi na hata wazazi wao walijua ni zamu yangu maana
walijua nilisimamia kila kitu mwenyewe kuanzia Kuhesabisha namba, kukimbiza
watoto mchakamchaka,kusimamia kufanya usafi wa mazingira,gwaride la asubuhi
utulivu madarasani na hata kazi za Elimu ya kujitegemea(E/K) nk.ukweli viranja
nao walibidi kufanya kazi kwa bidii zaidi.Naikumbuka sana kazi ya ualimu
Ndiyo!
Leo ni siku yetu walimu, katika kusherehekea siku hii, leo nimeiazimisha siku
hii na walimu wa Tarafa ya Siloka katika wilaya ya Bukombe katika kusherehekea
siku hii. Nimekumbuka mengi sana, nimeona walimu walivyosherehekea siku yao kwa
furaha kuu. Pamoja na mambo mengine nimewasikia wakidokeza kutokuthaminiwa na
jamii!Hapanikajifunza kitu Mbona hawathaminiwi?
Kazi
ya ualimu ni kazi ya uumbaji, ni kazi inayoanzisha maisha ya mwanadamu kwenye
ustaarabu wa dunia, hii ndiyo kazi iliyofanywa na mitume wa mwanzo kabisa
katika ulimwengu. Wote waliofanya kazi ya Ualimu wameacha alama ya kudumu
katika ulimwengu Huu. Akina Plato, Socrates, Aristotle, Alexander The Great,
Yesu Kristo, Mtume Muhamad na hata zama za akina Mahtma Gadhi hadi wa kati
Julius Nyerere. Wote hawa wanakumbukwa kwa kuacha alama kwenye maisha ya
ulimwengu na bila Shaka kwakuwa wote hawa walikua walimu.
Tunaposherehekea
siku hii walimu tutambue kazi yetu hii ni kiini cha Taaluma nyingine,
tusikubali mtu awaye yote akadunisha taaluma ama akatuona dhalili au tusio
muhimu. Nafahamu zipo changamoto nyingi zinazotukabili walimu ikiwemo madeni
mbalimbali yanatokanayo na mishahara na yale yasiyokua ya mishahara, nafahamu
mishahara ilipwayo kwa walimu bado ni midogo sana ukilinganisha na gharama
halisi za maisha. Hata hivyo ni vema tukatambua hakuna mtu atakaye kuja
kupigania hadhi yetu isipokua kuwa sisi wenyewe walimu.
Jamii
nayo kwa upande mwingine inatulaumu kutokana na vitendo vya wachache wetu,
ikiwemo ulevi, rushwa na hata kuwa na mahausiano ya mapenzi na wanafunzi mambo
haya yanapotendeka yanatupunguzia hadhi kwa jamii. Ni wajibu wetu sote kuonyana
na kushauriana kuwa pamoja na maisha binafsi tumebeba chapa ualimu wetu ambao
ni taaluma yetu sote.
Walimu
tunaposherehekea siku hii ya leo tutambue taifa hili linatutegemea sisi ndiyo
tunaoumba taifa, tukizalisha wahitimu wasiokuwa na maadili mema, tutambue kuna
wakati kwenye maisha ya Taifa letu tutakua na viongozi wasiokuwa na maadili
mema na kwa msingi huo taifa letu litapata matatizo makubwa tena pengine
kipindi ambacho hatutakuwepo ama tutakua tumezeeka sana hivyo watoto ama wajukuuzetu
watakua wahanga wa makosa tunayoyafanya leo.
Tunaposherehekea
tujitathimini je ni alama gani tutaacha kwa wanafunzi wetu? Tujiulize je tutakumbukwa
kwa jambo gani hata baada ya kustaafu? Je wanafunzi tunaofundisha wanafurahia
uwepo wetu madarasani? Na, je? Wanaelewa kwa kiwango cha juu yale tunayofundisha?
Walimu
wenzangu nawaomba sana tushirikiane kwa kila namna kumwondoa adui yetu mkubwa
ujinga, maradhi na magonjwa. Bahati njema maadui wote hawa huondolewa kwa
urahisi na Elimu ambayo sisi ndo tunaoitoa kwa watoto wa Taifa letu.
Tuendelee
bila kuchoka kukumbushana wajibu wetu na tuufanye wajibu huo kwa nguvu zetu
zote,ili tutakapokua tukidai haki zetu kusiwe na lawama yoyote kwetu. Wala
tusiangaliane kwa madaraja ya elimu zetu.
Natoa
wito kwa jamii ya kitanzania, ikumbuke kuwa mtu anaekaa kwa muda mrefu na mtoto
wako ni mwalimu. Maisha ya mtoto yanajengwa na mwalimu kwa kiasi kikubwa. Ni muhimu
na ni lazima ikiwa tunawapenda watoto wetu na Taifa letu basi tuwapende na kuwathamini
walimu wetu. Nimezisikia sauti za walimu zikipazwa juu ya kutokuthaminiwa na
Mimi kwa macho yangu jinsi baadhi ya jamii zinavyopuuza walimu, nimeona zaidi
ya mara mbili wazazi wakiwapiga walimu tena hadharani eti kwa sababu
hawakuhudhuria shughuli fulani ya kijamii, nimeona mara kadhaa wazazi wakienda
shuleni kupiga wa walimu eti kwa sababu watoto wao wameadhibiwa.
Matukio
Kama haya huwavunja moyo sana walimu.
Tunaposherekea
siku hii ya leo, niombe serikali iendelee kuwathamini walimu wa Tanzania. Iinue
hadhi ya mwalimu kwa kuwaondolea maudhi madogo mdogo mfano kuwalipa madei yao,
kujiepusha na utoaji wa kauli ambazo zinaweza kujenga dhana kwa jamii kwamba
kazi hii ni ya kawaida mno.
Mwalimu
day, ama siku ya mwalimu duniani impe nafasi kila mmoja wetu kutafakari anamthamini
vipi mwalimu. Tujikumbushe je ni mara ngapi tumeawatia moyo walimu wetu katika
kazi yao? Tujiulize hivi ni kweli tunaweza kusahau kwa haraka namna hii juu ya
mchango wa mwalimu kwenye maisha yetu? Ikiwa hatuwezi kuusahau mchango wa
mwalimukwenye maisha yetu, basi tutambue tuna deni kubwa kwa walimu wetu, na
deni lenyewe ni kuinua hadhi ya mwalimu.
Binafsi najitakia na
kuwatakia walimu wenzangu siku njema ya mwalimu duniani.
Mwl
Doto Biteko(mb)
Jimbo
la Bukombe.
Comments
Post a Comment