Madini wapania kuongeza mchango wao Pato la Taifa

Chanzo Halima Mlacha.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema hadi kufikia mwaka 2025, sekta ya madini nchini inapaswa ichangie asilimia 10 kwenye Pato la Taifa.

Katika kipindi cha mwaka 2015 sekta hiyo imechangia asilimia 4.3 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka 2014, kiasi ambacho waziri huyo amesema bado ni kidogo.

Aliyasema hayo mjini Dodoma jana mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akitoa taarifa kuhusu shughuli za utafutaji madini na maendeleo ya sekta ya madini.

Hata hivyo, alitaja changamoto zinazoifanya sekta hiyo kuwa na mchango mdogo katika Pato la Taifa kuwa ni pamoja na kushuka kwa bei ya madini kwenye soko la dunia na kutokuanzishwa kwa migodi mingine mikubwa ya uchimbaji hivi karibuni.

Alisema kwa sasa uwezo wa uzalishaji wa dhahabu kwa migodi yote nchini ni wakia milioni 1.25 kwa mwaka na uzalishaji kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 ni wakia milioni 5.68 sawa na tani 176.7 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 9.06 sawa na Sh trilioni 19.7.

Waziri huyo alifafanua kuwa ipo mipango mbalimbali ya kuendeleza shughuli za madini nchini ikiwemo kuboresha ukusanyaji na usambazaji wa taarifa na takwimu za kijiosayansi, udhibiti wa utoroshwaji wa madini na ukaguzi katika shughuli za uzalishaji madini.

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche alitaka kujua hatua zinazochukuliwa dhidi ya tuhuma za utoroshaji wa madini unaofanyika katika baadhi ya migodi ikiwemo mgodi wa Accacia ambao ndani ya mgodi kuna kiwanja cha ndege.

Comments