Said Ally akiwa na Diamond kwenye studio za Clouds FM
Mkuu wa
mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekuwa mstari wa mbele katika
kuhakikisha vitu alivyoviahidi kwa kijana Said Ally aliyetobolewa macho
maeneo ya Buguruni Sheli jijini Dar es Salaam anavipata. Alhamis hii,
ametimiza yote aliyoahidi na mengine.Katika
ahadi zake, Makonda aliahidi kumchangia Said shilingi milioni 10 na leo
hii amemkabidhi rasmi kiasi hicho. Pia amesema kupitia watu na taasisi
mbalimbali, atapewa pikipiki tano na Bajaji mbili. Kama hiyo haitoshi,
Makonda alisema kampuni ya GSM imeahidi kumnunulia nyumba kijana huyo .“Nimeleta
milioni 10 zangu siwezi kusahau lakini hili namuachia mwenyezi Mungu,
naomba nikukabidhi, nashukuru na wale walioniunga mkono katika kumpatia
Bodaboda 5 na Bajaj mbili ambazo zimetoka katika makampuni tofauti
tofauti,” alisema Makonda.
“Jambo
ambalo nilikuwa nikimlilia Mungu anipe nafasi ili niweze kulifanikisha –
ni jambo ambalo lilikuwa likimsumbua kila mtu, ni jambo la Said kupata
kiwanja na ukiangalia kwenye mji wetu huu kiwanja kinauzwa kwa bei ya
juu sana, vinginevyo utaenda Magwepande na bado utakuwa nje ya mji,”
aliongeza.
Milioni 10 mezani: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akijiandaa kumkumbatia Said Ally. Kushoto ni mama yake mzazi
“Shughuli
za kibiashara zinafanyika katika ya mji, na hili jambo ulilisema
ofisini kwangu na mimi nilikuwa nikimlilia Mungu anipe nafasi ya
kufanikisha ndoto yako. Tumepata mdau ambaye amekubali na kumnunulia
ndugu yetu Said nyumba, ambayo ni kampuni ya GSM na nimewambia
wasikupeleke Magwepande, wasikupeleke Bunju, Mbagala, Gongo la Mboto.
Nataka ukae mazingira yale yale ambayo umeyazoea. Iwe Tabata unakuja
tena Buguruni, Mwenge. Nataka maeneo haya haya ambayo watu wamezoea
kukuona. Kwahiyo ndugu zetu wa GSM wamekubali kuniunga mkono kumnunulia
nyumba. Mi nakuombea neema ya bwana iendelee kutembea katika maisha
yako,” alisisitiza Makonda.

Said Ally akizungumza jambo
Kwa
upande wake, Said alishukuru na kusema, “Ukiona mtu anatoa chozi
kwaajili ya mwananchi wake ni jambo zuri, alivyosikia kwenye vyombo vya
habari hakuchelewa kuja. Lakini leo nashukuru sana kwa kila kitu
alichonitendea, nashukuru sana.”
“Sina cha
kumlipa zaidi ya kumuombea dua siku nyingine nisikie amekuwa waziri.
Nashukuru sana namuombea kila siku na watu siwezi kuwasahau sana, Clouds
ni watu ambao sitawasahau sana na Diamond sitamsahau sana,” alisema.
Wakati
huo huo wahenga wanasema ‘milima haikutani lakini binadamu hukutana.’
Hii likuwa kwa Said ambaye alipenda siku moja amuone mwanamuziki
anayemkubali zaidi, Diamond Platunumz.
Said
alishindwa kuvumilia baada ya kusikia wimbo wa Salome na video yake
ambayo hajawahi kuiona na mbele ya msanii Diamond aliyekuwa akimpenda,
hatimaye leo wamekutana. Amedai kukutana na Diamond wakati hana uwezo wa
kumuona ni kitu kinachomuumiza lakini amefurahi.
Staa huyo anayemiliki label ya WCB, alitoa shilingi milioni mbili za kumkabidhi Said aliyezipokea kwa furaha.
Comments
Post a Comment