TPSF YATOA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI MKOANI GEITA

Katibu Tawala wa wilaya ya Geita Thomas Dimme akifungua semina ya wajasiriamali ya taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation iliyofanyika wilayani humo

Mkuu wa kitengo cha wajasiriamali kutoka kutoka mfuko wa kuendeleza sekta ya fedha (FSDT) akiongea wakati wa mafunzo hayo.

Afisa Mwandamizi kutoka ofisi ya RAS ya Geita akiongea wakati wa mafunzo hayo.

Ni meneja Mradi wa mafunzo kutoka TPSF, Celestine Mkama,akitoa maelekezo kwa wanasemina

Baadhi ya wajasiriamali waliohudhuria mafunzo mafunzo hayo wakifuatilia mada mbalimbali kutoka kwa wakufunzi.
Wajasiriamali waliopo mkoani Geita wametakiwa kutumia raslimali mbalimbali zilizopo mkoani humo na firsa zinazojitokeza kwa sasa kuibua miradi ya biashara na kuendesha biashara yao kitaalamu wakiwa na malengo ya kujikwamua kutoka katika hali ya umaskini.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Tawala wa wilaya ya Geita,Bw.Thomas Dimme aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo kama mgeni rasmi wakati wa mafunzo maalumu ya mbinu za kuendeleza wajasiriamali yaliyoandaliwa na taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation.
Bw.Dimme alisema kuwa serikali imefungua milango ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kwa kutumia fursa zilizopo hivyo aliwataka kuibua miradi ya biashara na kuwa na utayari wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika biashara kwa kipindi hiki mojawapo ikiwa ni ushindani mkubwa na kufanya biashara kwa kufuata njia halali zinazotakiwa ikiwemo kulipa kodi za serikali kwa mujibu wa sheria.
Aliipongeza taasisi ya TPSF kwa kuendesha miradi ya mafunzo kwa wajasiariamali sehemu mbalimbali nchini “Nawapongeza kwa kuwafikishia mafunzo wajasiriamali wa ngazi za chini katika ngazi ya mikoa na wilaya kwa kuwa wafanyabiashara wakipata mafunzo kama haya kwa vyovyote wataweza kupata mafanikio katika shughuli zao”.Alisema Dimme.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Mafunzo kutoka taasisi ya TPSF,Celestine Mkama alisema kuwa taasisi hiyo inaendesha mradi wa kuwapatia mafunzo wajasiriamali kuhusiana na mbinu mbalimbali za kufanya biashara kwa lengo la kupata mafanikio.
“Mafunzo haya yamelenga kuwapatia maarifa wafanyabiashara wadogo ili yawajengee uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizopo katika biashara “Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa wakikosa mbinu za kufanya biashara kutokana na kukosa elimu ya biashara ndio maana tumeona tuwasaidie katika eneo hili la kuwajengea uwezo kupitia kuwapatia elimu ya ujasiriamali”.Alisema Bw.Mkama.
Mkama alisema baadhi ya masuala yanayofundishwa kupitia mafunzo haya ni utunzaji wa mahesabu ya biashara, nidhamu katika matumizi ya fedha,utunzaji wa kumbukumbu za biashara na jinsi ya kupanga miradi.
Akiongea kwa niaba ya wajasiriamali wenzake,Bi.Elizabeth Bigambo ,aliishukuru taasisi ya TPSF kwa kuwafikishia elimu ya ujasiriamali. “Tuna imani mafunzo haya tuliyoyapata yatatusaidia katika kukuza biashara zetu na kukua kibiashara na kuchangia pato la taifa kwa njia ya kodi”.Alisema Bigambo

Comments