SIMIYU YAJIPANGA KUANZA KUTENGENEZA CHAKI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akionesha aina tofauti za maboksi yatakayotumika kufungashia chaki nyeupe na za rangi ambazo zinatarajiwa kuanza kuzalishwa na Vijana wa Wilaya ya Maswa, Mkoani humo wakati alipohitimisha Mafunzo ya Teknolojia ya Utengenezaji wa Chaki kwa vijana hao, (katikati) Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Seif Shekalaghe (kulia) Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa, Mhe. Peter Bunyongoli.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Seif Shekalaghe akizungumza na vijana na wadau wengine wakati wa kuhitimisha mafunzo Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo SIDO kwa Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa, katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Meneja wa Shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga, Athanas Moshi (aliyesimama) akizungumza na vijana na wadau wengine wakati wa kuhitimisha mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na Shirika hilo  kwa Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa.

Baadhi ya Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa wakiangalia sampuli za maboksi yaliyopendekezwa kutumika kufungashia chaki pindi uzalishaji utakapoanza wakati Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) akihitimisha mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na SIDO kwa vijana hao, wilayani humo
Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa wakiweka chaki walizotengeneza wakati wa mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na SIDO katika maboksi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) kabla ya Mkuu huyo wa mkoa  kuhitimisha mafunzo hayo. 
 Na Stella Kalinga, Simiyu
Serikali Mkoani Simiyu imetangaza azma yake ya  kuanza kutengeneza Chaki ambazo zitauzwa katika Wilaya za Mkoa huo na nchi nzima kabla ya Oktoba 14 mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony John Mtaka wakati alipohitimisha mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji wa Chaki kwa vikundi vya vijana Wajasiriamali wilayani Maswa, yaliyotolewa na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga.
Mtaka amesema shule zote za Msingi na Sekondari za Serikali Mkoani humo  zinatumia jumla ya katoni 1200 za chaki ambazo zinagharimu shilingi 25,000,000 kwa kila mwezi, hivyo kama Vijana wa Wilaya ya Maswa wakizalisha Chaki na kusambaza katika mkoa mzima watajipatia kipato na kuondokana na umaskini.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na Tanzania ya Viwanda, Mkoa huo umejipanga kuimarisha uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo ambavyo vitazalisha mahitaji ya kila siku ya wananchi, hivyo wamedhamiria kuwa na uzalishaji wa bidhaa moja kwa kila wilaya ( one district  one product), ambapo Wilaya ya Maswa itakuwa ikizalisha chaki.
“Wilaya ya Maswa imepokea shilingi 38,000,000  Meatu 31,000,000 kwa ajili ya vijana kutoka Wizara yenye dhamana na Vijana, sasa hivi  tumepeleka maombi ya wilaya zilizobaki. Tumedhamiria kuutambulisha Mkoa kwa kuzalisha bidhaa zetu wenyewe, tumeanza na Chaki wilaya ya Maswa, Wilaya ya Meatu wao watazalisha maziwa,  tutaendelea kutengeza utambulisho(brand) wa wilaya nyingine kwa kuzalisha bidhaa zinazoendana na malighafi zilizopo” alisema Mtaka.
Akizungumza katika hitimisho la Mafunzo hayo kwa Vijana, Meneja wa Shirika la Viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga, Athanas Moshi ametoa wito kwa vikundi vya vijana kuwa na mipango itakayowasaidia kutangaza bidhaa zao na kupata soko la bidhaa hizo ndani na nje ya Mkoa ili kujiongezea kipato.
“Mtakapoanza kuzalisha chaki, kulingana na tathmini iliyofanyika kama mtauza kwa Mkoa wa Simiyu tu mtakuwa na uwezo wa kutengeneza faida ya shilingi 8,000,000 kila mwezi, hiyo si fedha ndogo mkiwa na mipango thabiti mkazalisha chaki bora mtaweza kuuza chaki zenu nchi nzima na hata nje ya nchi” alisema Moshi.
Naye mmoja wa vijana waliopata mafunzo ya utengenezaji wa chaki, Kelvin Steven ametoa wito kwa Wananchi wa  Simiyu na Watanzania kwa ujumla,  kuunga mkono juhudi za Vijana Wajasiriamali na kuthamini bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kuinua uchumi wa Vijana hao na Taifa kwa jumla.
Aidha, Bi. Specioza Fundikira ambaye pia amepata mafunzo hayo amesema matarajio ya Vijana waliopata mafunzo ni kuwa uzalishaji wa chaki utakapoanza kutakuwa na soko la uhakika kwa Shule zote za Msingi na
Sekondari za Serikali mkoani humo na mikoa ya jirani, vijana watapata ajira na kuachana na shughuli zisizo halali kama wizi na ulevi.
Kwa Mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Seif Shekalaghe vijana kutoka vikundi 8 vya Wajasiriamali ambao wameunda kikundi kimoja cha ‘Maswa Youth Enteprises’ wamepatiwa mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji wa chaki na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga kuanzia tarehe 29/08/2016 hadi tarehe 03/09/2016

Comments