CWT Arusha yampa Mkurugenzi siku 14 kuhusiana na walimu kuvuliwa madaraka


Tokeo la picha la nembo ya chama cha walimu tanzania

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Arusha, kinakusudia kuandaa maandamano yasiyokuwa na kikomo endapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Athuman Kihamia, hatafanya mazungumzo na walimu wakuu na waratibu elimu 33 waliovuliwa madaraka -- MTANZANIA limeripoti.

Pia kimetoa siku 14 kwa Kihamia kutengua barua za kuwavua madaraka walimu hao kwa tuhuma za kuwa na wanafunzi hewa na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 27.

Akitoa tamko la kupinga kuvuliwa madaraka walimu hao mjini hapa jana, Kaimu Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Arusha, Andrew Ngazu, alisema walimu hao walivuliwa madaraka kwa kuonewa kwa sababu hawakusikilizwa na mwajiri wao huku wakiwa hawajashirikishwa.

Alisema CWT wanaunga jitihada za Rais Dk. John Magufuli za kuhakiki ili kubaini shule zenye wanafunzi hewa ila wanapinga jinsi mpango huo ulivyoendeshwa katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.
“Tunampa siku 14 atengue barua za kuwavua madaraka walimu na waratibu hao, tutakuwa tayari kukaa meza moja ya majadiliano na mkurugenzi huyo kwa ajili ya suala hilo iwapo atakubali kutengua barua hizo kwanza.
“Asipofanya hivyo tutafanya maandamano ya walimu wa shule za msingi na sekondari za halmashauri ya jiji pamoja na wilaya za jirani, maandamano yasiyo na kikomo hadi mkurugenzi atakapowasikiliza walimu hao wakijitetea,” alisema Ngazu.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa CWT Mkoa wa Arusha, Nurueli Kavishe, alisema wamejiridhisha pasipo shaka kuwa walimu hao wameonewa kwa sababu katika orodha ya wanafunzi hao kuna waliohama ila wanaitwa wanafunzi hewa.

Alisema idadi ya wanafunzi hubadilika kwa sababu kuna waliohama, wengine wanahamia na wanaomaliza shule hivyo lazima idadi itofautiane kuhakiki wanafunzi na Serikali haijawahi kutoa maelekezo kuwa akihama fedha zake zipelekwe wapi.
“Mkurugenzi aunde tume huru atushirikishe na sisi ili tupitie suala hili, asionewe mtu na asipofanya hivyo tutaenda kuandamana kwa sababu wenzetu wamedhalilishwa bila kushirikishwa,” alisema Ngazu.
Naye Mwenyekiti wa CWT Jiji la Arusha, Grace Msaki, alisema suala la wanafunzi hewa limewaathiri walimu huku wengine hivi sasa wakipita njiani wanaitwa wezi.

Comments