Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Aapa Kukomesha Lumbesa


WAZIRI Mkuu, Kasim Majaliwa, ametoa onyo kwa wafanyabiashara wanaodhulumu wakulima kwa kununua mazao kwa kuyafunga kwenye magunia bila kuzingatia vipimo sahihi maarufu kama lumbesa, na kutaka viongozi kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mikoa kusimamia.

Alisema serikali itapambana na wafanyabiashara wanaoendelea kulazimisha kufungasha mazao katika magunia bila kuzingatia vipimo sahihi hivyo kuwapunja na kuikosesha serikali mapato.

Akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Saumu Sakala (CUF) katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Majaliwa alikiri kuwa serikali ilishazuia matumizi ya kipimo cha lumbesa na kuahidi kwamba awamu hii, itakomesha dhuluma hiyo.

Awali mbunge huyo alitaka kauli ya serikali dhidi ya vitendo hivyo kuendelea ingawa kupitia viongozi mbalimbali wa serikali, vilishapigwa marufuku.

Waziri Mkuu alitoa mwito tena kwa wakuu wa wilaya, halmashauri zao, maofisa biashara katika halmashauri hizo kuhakikisha unyonyaji huo unakomeshwa.

“Jambo hili wala siwaachii wakuu wa wilaya peke yao bali nawaagiza hata wakuu wa mikoa kupitia kamati zao za ulinzi na usalama kuhakikisha agizo hili linatekelezwa, swali hili la mbunge linaashiria mambo haya bado yanafanyika,” alisema.

Pia aliwaagiza watendaji wa vijiji na kata, kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanaouza mazao kwenye maeneo yao, hawauzi mazao kwa kipimo cha lumbesa.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema tayari maelekezo yametolewa kwa Wakala wa Vipimo, kuhakikisha biashara yote ya mazao ya kilimo nchini yanauzwa kwa vipimo vya kilogramu na siyo kwa kufungashwa lumbesa.

Alisema ingawa kuna vijiji visivyokuwa na mizani, hali hiyo siyo kigezo cha kuhalalisha lumbesa, badala yake alisema magunia yote nchini yametengenezwa kwa vipimo hivyo mazao yanapojazwa gunia lazima lifungashwe kwa kushonwa kwa uzi au kamba.

Comments