Upinzani Burundi Wataka AU,EU wasishiriki mazungumzo ya kutafuta amani

Mzunguko wa kwanza wa mazungumzo ya Burundi umemalizika, huku kukiwa na mvutano kuhusu kualikwa kwa chama cha CNARED, kinachojumuisha wanasiasa wanaoishi nje ya Burundi. 

Msuluhishi wa mgogoro huo, Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa alisema mzunguko wa kwanza ulijikita zaidi katika ‘mazungumzo binafsi’ na Serikali. 

Alisema mzunguko wa pili utaanza mwishoni mwa mwezi ujao na kwamba atakutana na vikundi ambavyo havikuhudhuria mzunguko huo, akiamini vitakuwa na mchango wenye masilahi. 

Burundi imekuwa kwenye mgogoro huo baada ya uchaguzi uliopita na zaidi ya watu 450 wameuawa tangu Rais Pierre Nkurunziza alipogombea kipindi cha tatu cha urais na kushinda. 

Wapinzani wake wanadai kugombea kwake kumevunja Katiba inayotamka vipindi vya urais ni viwili. Mzunguko wa kwanza wa mazungumzo hayo ulianza mwishoni mwa wiki jijini Arusha, baada ya majadaliano ya mwaka jana kabla ya Mkapa kuteuliwa, yaliyofanyika kwa nyakati tofauti katika nchi za Burundi na Uganda kushindikana. 

Hata hivyo, baadhi ya vikundi vya upinzani kikiwamo cha CNARED, kinachojumuisha wanasiasa na maofisa wa zamani wa Serikali wanaoishi uhamishoni, walisema mazungumzo hayo yanahitaji kujumuisha wapinzani wote.

“Mazungumzo lazima yawe kati ya upande wa Nkurunziza na vyama vyote vya upinzani na vikundi vya kijamii wanaopinga muhula wa tatu.”alisema msemaji wa CNARED, Pancrace Cimpaye. 

Wakati huohuo; vyama tisa vilivyoshiriki uchaguzi wa Burundi wa mwaka 2015 , vimetaka wawakilishi wa umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika kutoshiriki katika mazungumzo ya amani ya Burundi. 

Katika taarifa yao iliyotiwa sahihi na viongozi wote tisa wa vyama hivyo, walisema kutokana na lugha na misimamo ya wawakilishi hao wa taasisi za juu, ni wazi wataharibu mchakato huo unaoendelea wa kutafuta amani ya Burundi.

Viongozi hao wamemtaka msuluhishi wa mgogoro huo, Rais mstaafu Mkapa kutokubaliana na wawakilishi hao na kushirikisha pande zote zenye masilahi na mgogoro wa Burundi.

Comments