Mkuu wa Mkoa na Waziri Kitwanga Watofautiana Kuhusu Kuwepo Kwa Tawi la Magaidi wa Al Shabaab na Islamic State (IS) jijini Tanga

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Charles Kitwanga na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela wametofautiana juu ya taarifa za kuwapo kwa tawi la kundi la kigaidi la Islamic State (IS) jijini Tanga

Juzi, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC Swahili) lilitangaza uwepo wa watu waliojitambulisha kuwa wawakilishi wa kundi hilo wanaoendesha operesheni kwa nchi za Afrika Mashariki.

Shirika hilo lilieleza kuwa kundi hilo limetuma ujumbe na kujitambulisha kwa kutumia video ya dakika moja waliyoituma kwenye mtandao wa Twitter na kuzungumza na Waziri Kitwanga ambaye alithibitisha kuwa na taarifa hizo.

“Tumezisikia na tumechukua hatua. Askari wetu wanafanya operesheni,” alikaririwa Waziri Kitwanga.

Hata hivyo, jana Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela aliwaambia waandishi wa habari, kuwa mauaji na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yaliyotokea mfululizo katika maeneo mbalimbali jijini hapa siku za karibuni hayahusiani na ugaidi.

Alifafanua kuwa wahalifu waliopo huko wamegundulika kuwa wahamiaji haramu kutoka Ethiopia, ambao wanaingia nchini kwa kutumia vichochoro vilivyoko kwenye mapori ya mpaka wa Kenya na Tanzania, wakielekea nchi jirani. Wamekuwa wakiingia nchini kupitia baadhi ya maeneo ya wilaya ya Mkinga.
 
Wahalifu hao hutumia mapango hayo, kujificha kwa muda wakati wakisubiri kuendelea na safari yao kuelekea nchi za Kusini mwa Afrika. 

“Napenda kuwajulisha wakazi wa Tanga na taifa kwa ujumla kwamba hapa mkoani hatuna vita dhidi ya kundi lolote la ugaidi wala kikosi cha Al-Shabaab, isipokuwa kuna operesheni maalumu ya kikosi kazi chetu cha ulinzi na usalama, kinachopambana na mambo makuu matatu; kubwa ni matukio ya uhalifu unaofanywa na wahamiaji haramu,” alisema Mkuu wa Mkoa.
 
Alisema kamati ya ulinzi na usalama mkoa, baada ya kutafakari mwenendo wa kiusalama kutokana na matukio ya uhalifu wa hapa na pale, imeunda kikosi kazi kukomesha vitendo hivyo, vinavyofanya mkoa kutumiwa kama uchochoro.
 
Shigela ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, aliyataja mambo yanayoshughulikiwa na kikosi kazi hicho ni kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya, magendo ya bidhaa zisizoruhusiwa au kuingizwa bila kufuata utaratibu pamoja na wahamiaji haramu.
 
“Wahamiaji haramu ndilo jambo hatarishi sana hapa kwa sasa, kwa sababu hao watu wakishaingia nchini kwa njia za panya na kufanikiwa kujificha, basi wanaposikia njaa hulazimika kujitokeza mitaani kutafuta chakula kwa kuvamia maduka, kama walivyofanya katika duka kuu la Central Bakery mwishoni mwa mwezi uliopita”, alisema.
 
Akizungumzia wakazi wa Kata ya Amboni yaliko mapango na mapori husika, aliwataka kuchukua tahadhari, hasa wale wanaofanya shughuli za kilimo jirani, kwa kuacha kuwenda kwa muda maeneo hayo, hasa kipindi hiki ambacho kikosi kazi kinaendeleza operesheni.

Comments