Bomba la Mafuta Kutoka Uganda Kuongeza Ajira

Serikali  imetaja manufaa ya mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania kuwa miongoni ni kuongezeka kwa uwekezaji wa fedha za kigeni na fursa za ajira.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliambia Bunge jana kuwa Aprili mwaka huu, Tanzania ilisaini Makubaliano ya Awali (MoU) na Serikali ya Uganda kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Alisema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,443 ambazo kati ya hizo, kilometa 1,115 zitakuwa upande wa Tanzania.

“Bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 200,000 ya mafuta ghafi kwa siku,” alisema Profesa Muhongo akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2016/17 yanayofikia Sh 1,122,583,517,000.

Aliyataja manufaa ya bomba hilo kwa Tanzania kuwa ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kupitia Bandari ya Tanga, tozo ya kupitisha mafuta ghafi kwenye bomba na ajira za kudumu kwa Watanzania 1,000 na 10,000 za muda.

Alisema majadiliano ya utekelezaji wa mradi huo kati ya Serikali za Tanzania, Uganda, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na kampuni za Total (Ufaransa), CNOOC (China) na Tullow (Uingereza) yameanza.

Alisema katika kuimarisha ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Uganda imealika nchi za Burundi, Kenya, Rwanda na Tanzania kushiriki katika uwekezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi nchini Uganda.

Comments