Mbunge wa Kavuu, Dk Prudenciana Kikwembe (CCM) ameitaka Serikali kueleza ni lini itatoa fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa wakati.
Dk Kikwembe akiuliza swali la nyongeza bungeni, alisema mara nyingi fedha za maendeleo zimekuwa zikipelekwa katika maeneo husika kwa kuchelewa na hivyo kuchelewesha miradi mingi.
“Ni lini fedha za utekelezaji wa shughuli za maendeleo zitatolewa kwa wakati na fedha zinapochelewa na kutolewa mwishoni mwa mwaka wa fedha, fedha hizo huwa zinaenda wapi?”Alihoji Dk Kikwembe.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo alikiri kuwa miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikisuasua kutokana na ukosefu wa fedha.
Hata hivyo alisema, kutokana na jitihada zilizopo za kukusanya mapato ya Serikali, tayari baadhi ya miradi iliyokwama imeshaanza kutekelezwa na anaamini miradi yote iliyokuwa imekwama itatekelezwa kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha.
Awali, katika swali la msingi Mbunge huyo alitaka kujua ni lini kata ya Mamba, Majimoto, Chamaledi na Mwampuli zitapatiwa maji safi na salama .
Akijibu swali hilo Jaffo alisema ili kutatua changamoto ya maji katika kata ya Mamba, Serikali imetenga Sh milioni 24 katika bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu katika kijiji cha Ntaswa ambacho hakina maji kati ya vijiji vilivyopo.
Alisema vijiji ambavyo havijapata huduma ya maji katika kata ya Majimoto ni Kuchimba na Ikulwe ambavyo alisema vimetengewa Sh milioni 48.4 katika bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa ajili ya kuchimba visima virefu kila kijiji.
Comments
Post a Comment