Mwanamke alieolewa na wanaume wamili afariki dunia - KATAVI

image001
Marehemu Veronica Salehe (54), mkazi wa Kijiji cha Ikondamoyo Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele mkoani hapa aliyewahi kuripotiwa kuolewa na wanaume wawili  akiwa na wanaume hao.
MWANDISHI WETU, KATAVI

Ameacha simanzi! Kifo cha mwanamke, Veronica Salehe (54), mkazi wa Kijiji cha Ikondamoyo Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele mkoani hapa aliyewahi kuripotiwa kuolewa na wanaume wawili tofauti na taratibu zilizozoeleka aliyeishi nao kwa kipindi cha miaka tisa, kimeacha simanzi nzito kwa wanaume hao.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikondamoyo, John Maganga, kifo hicho kilichotokea hivi karibuni mkoani Tabora ambako Veronica alikuwa amekwenda kupatiwa matibabu kwa kaka yake, kimefanya wanakijiji wa kijiji hicho kubaki na mshtuko kwani kilikuwa cha ghafla na kwamba wanaume hao wamepata pigo kubwa.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa, katika uhai wake, aliishi vizuri na wanaume hao, Paulo Sabuni (62) (mume mkubwa) na Arcado Mlele (47) (mume mdogo) hivyo kuwashangaza wengi ndiyo maana kifo chake kimekuwa habari inayozungumzwa na wengi.
Ilielezwa kwamba, umaarufu wa Veronica kijijini hapo ulitokana na shughuli za kilimo na biashara ya pombe ya kienyeji aina ya komoni alizokuwa akijishughulisha nazo.
“Kiukweli kifo chake kimewagusa wengi kwa sababu alifanya kitu cha tofauti cha kuweza kuhudumia ndoa mbili na kila mwanaume akawa sawa bila kuhitilafiana na mwenzake, jambo ambalo kwa wengine ilionekana kitu kisichowezekana,” alisema mmoja wa wanakijiji hao na kuongeza:
“Hata hivyo, ndoa na mume mdogo ilivunjika mwaka jana.”

Veronica alibahatika kuwa na watoto wanne, wawili wa kike, mmoja wa kiume akiwa ni wa mume mdogo na wengine wa mume mkubwa.
Katika shughuli za msiba wa Veronica, wanaume hao walishirikiana hadi wakamaliza msiba huo ambapo mazishi yalifanyika kijijini hapo nyumbani kwa baba wa marehemu, Salehe.

Comments