DKT. BITEKO AWATAKA WANANCHI KUISHI KWA UPENDO


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa, Dkt. Doto Biteko, amewataka wananchi kuendelea kuishi kwa upendo, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayeweza kujitosheleza peke yake katika maisha.

Dkt. Biteko ametoa wito huo wakati akitoa salamu za pole katika msiba wa Diwani wa Kata ya Ilolangulu, Kabula Ndabacha, aliyefariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini.

Amesema jamii inapaswa kuthaminiana, kusaidiana na kuishi kwa upendo katika nyakati zote, akitumia mfano wa simu ya gharama kubwa ambayo, pamoja na thamani yake, haiwezi kufanya kazi bila laini ya simu.

“Hata ungenunua simu ya bei kubwa kiasi gani, bado inahitaji laini ya shilingi 2,000 ndipo ikamilike,” alisema Dkt. Biteko.Ameeleza kuwa mfano huo unaonyesha umuhimu wa kila mmoja kumhitaji mwenzake, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kujenga upendo, mshikamano na kusaidiana katika maisha yao ya kila siku.

Ujumbe huo wa Dkt. Biteko uliwagusa kwa kiasi kikubwa waombolezaji waliohudhuria msiba huo, wakiwemo wanafamilia, viongozi na mamia ya wananchi waliojitokeza katika eneo la Ilolangulu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Fagasoni Nkingwa, ameiomba familia ya marehemu kuendelea kudumisha upendo na mshikamano aliouacha marehemu Kabula Ndabacha.Nkingwa, akitoa salamu za pole kwa familia na wananchi wa Ilolangulu na kumuombea marehemu apumzike kwa amani, amesema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza katika mazishi hayo ni ushahidi wa upendo, heshima na mchango mkubwa ambao marehemu aliutoa kwa jamii katika kipindi cha uhai wake na wakati wa uongozi wake.

Msiba huo pia ulihudhuriwa na madiwani wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, jambo lililoonyesha mshikamano, upendo na ujirani mwema katika kipindi hiki cha majonzi.


Akizungumza kwa niaba ya madiwani wa Halmashauri ya Mbogwe, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Enock Magulu, amesema wamepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa, wakimtaja marehemu Kabula Ndabacha kuwa alikuwa diwani aliyewakilisha vyema wananchi wake na mtetezi wa maslahi yao.

Magulu amesema marehemu ameacha kumbukumbu nzuri kupitia utendaji wake wa kazi, uwakilishi na namna alivyowahudumia wananchi, akieleza kuwa mchango wake utaendelea kukumbukwa na jamii.

Ameongeza kuwa madiwani wa Halmashauri ya Mbogwe wameungana na familia, ndugu, jamaa, viongozi na wananchi wa Ilolangulu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, huku wakimuombea marehemu apumzike kwa amani.


Comments