MAMA ANAYETUHUMIWA KUMFUKIA MTOTO MCHANGA AKIWA HAI AKAMATWA GEITA

 
Na, Ernest Magashi

ebukombesasa.blogspot.com.tz

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mkazi wa Kijiji na Kata ya Muungano, Wilaya ya Chato, Amina Shabani (21) kwa tuhuma za kumfukia mtoto wake mchanga wa jinsia ya kike akiwa hai ndani ya shimo muda mfupi baada ya kujifungua.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, alisema tukio hilo lilitokea Mei 16, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri nyumbani kwa mtuhumiwa, saa chache baada ya kujifungua.
Kamanda Jongo alisema mtuhumiwa alijifungua siku hiyo majira ya saa 4:00 asubuhi, huku tukio hilo likibainika Mei 17, 2026 majira ya saa 1:00 usiku baada ya wananchi kusikia sauti ya mtoto mchanga kutoka nyuma ya nyumba ya mtuhumiwa bila kumuona mtoto huyo.


Alisema baada ya taarifa kutolewa, Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kumuokoa mtoto huyo akiwa hai, kisha kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa ajili ya uchunguzi na matibabu. Hata hivyo, mtoto huyo alifariki dunia Mei 18, 2026 majira ya saa 10:00 alasiri akiwa anapatiwa matibabu.

Aidha, baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia na kujificha kwa lengo la kukwepa mkono wa sheria. Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kubaini alikokuwa amejificha na kumkamata akiwa katika harakati za kutorokea mkoa jirani.
Kamanda Jongo alisema chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa, na uchunguzi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.


Pia ametoa wito kwa wananchi kuimarisha malezi na uangalizi kwa wanawake wajawazito na waliojifungua ili kuhakikisha wanapata msaada wa kijamii, kisaikolojia na kiafya kwa wakati, ikiwemo kuwahi kupata huduma za hospitali.
 

Comments