Na, Ernest Magashi
Wananchi wa Kata ya Butinzya, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wametakiwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kujitolea nguvu kazi na kuchangia rasilimali zao.
Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Dkt. Doto Biteko, wakati wa ziara yake ya kuwashukuru wanachama kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe pamoja na madiwani.
Dkt. Biteko alisema kuwa maendeleo ya Bukombe yanategemea mshikamano wa wananchi, akisisitiza kuwa endapo wataendelea kushirikiana, wilaya hiyo itapiga hatua kubwa zaidi ya ilivyo sasa.
“Bukombe ya leo ni bora, lakini inaweza kuwa bora zaidi ikiwa tutaungana na kushirikiana katika miradi ya maendeleo,” alisema Dkt. Biteko.
Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta fedha za maendeleo zinazowezesha utekelezaji wa miradi katika sekta za elimu, maji, afya pamoja na ujenzi wa barabara ya lami ya Ushirombo Katoro.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Mathias, alimpongeza Dkt. Biteko kwa ushirikiano wake na wananchi katika kuchochea maendeleo, ikiwemo kuchangia ujenzi wa zahanati.
Mathias alisema kupitia juhudi za mbunge huyo, serikali imetoa shilingi milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Iponyazala, huku wananchi wakiendelea kujitolea nguvu kazi katika kusogeza mbele maendeleo ya eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja, alimpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi zake za kuhamasisha maendeleo na kuimarisha mshikamano kati ya chama na wananchi.

Comments
Post a Comment