Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi trilioni moja katika utekelezaji wa miradi ya gesi asilia mkoani Mtwara, kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa gesi nchini.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo, Ndejembi amesema miradi inayotekelezwa ni pamoja na uchimbaji wa visima vya gesi katika eneo la Ntorya, ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Ntorya hadi Madimba, pamoja na uchorongaji wa visima katika Kitalu cha Mnazi Bay. Amesema miradi hiyo itaongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa gesi kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwandani na majumbani.
“Uwekezaji katika miradi hii ni mkubwa na Serikali imetoa kipaumbele maalum kwa sekta ya gesi asilia. Mahitaji ya gesi yanaongezeka kwa kasi kadri idadi ya wateja inavyoongezeka. Hivyo, changamoto hii ichukuliwe kama fursa kwa kushirikiana na wabia na wakandarasi ili miradi ikamilike kwa kasi na ufanisi,” amesisitiza Ndejembi.
Waziri huyo ameelekeza kuwa kuanzia Septemba 2026, uzalishaji wa gesi katika eneo la Ntorya uanze rasmi ili kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuchochea shughuli za kiuchumi, hususani katika Ukanda wa Kusini na maeneo mengine ya nchi.
Amebainisha kuwa jitihada hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kutoa fedha na miongozo madhubuti kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Aidha, Waziri Ndejembi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza utafiti na uchimbaji wa visima vipya ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha nchi inanufaika kikamilifu na rasilimali zake za gesi.
Pia ameliagiza Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) kuhakikisha linaimarisha mpango wa kurejesha faida kwa jamii (CSR) kwa kushirikiana na halmashauri husika, ili wananchi wanaozunguka maeneo ya miradi ya gesi wanufaike moja kwa moja na uwekezaji huo kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Comments
Post a Comment