Watendaji na wataalamu wa ngazi ya kata pamoja na vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wa kutumia mfumo wa kidijitali wa e-Mrejesho, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo yalifanyika Machi 3, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, yakihusisha wataalamu kutoka kata mbalimbali. Lengo kuu lilikuwa kuwapa ujuzi wa kupokea, kuchakata na kutoa mrejesho wa malalamiko, pongezi, ushauri na hoja zinazowasilishwa na wananchi kwa wakati kupitia mfumo huo.
Akitoa mafunzo hayo, Mratibu wa e-Mrejesho Wilaya ya Bukombe, Yusuph Mwaipalu, alisema kuwa matumizi ya mfumo huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha utawala bora kwa kuhamia katika mifumo ya kidijitali, ili kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao.
Alisisitiza kuwa watendaji wanapaswa kuyatumia mafunzo hayo kama chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao ya kazi.
“Mfumo huu utasaidia kupunguza ucheleweshaji wa majibu kwa wananchi, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji katika ngazi ya kata na kijiji. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunautumia ipasavyo kwa manufaa ya wananchi,” alisema Mwaipalu.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kuhakikisha huduma za umma zinaboreshwa kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa ya TEHAMA.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Ramadhani Ng’oi aliipongeza Halmashauri kwa kuona umuhimu wa kuwajengea uwezo wataalamu wake, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya utatuzi wa changamoto za wananchi na kuimarisha imani yao kwa Serikali.

Comments
Post a Comment