WASIMAMIZI WA CHANJO YA MATONE YA POLIO WAJENGEWA UWEZO BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

Wasimamizi wa utoaji wa chanjo ya matone ya Polio (nOPV2) katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamepatiwa mafunzo maalum ya namna bora ya kusimamia na kutekeleza zoezi la utoaji chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10.Mafunzo hayo yalifanyika Machi 14, 2026 yakitolewa na wataalamu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, yakiwa na lengo la kuimarisha maandalizi ya kampeni ya chanjo pamoja na kuzuia maambukizi ya virusi vya Polio katika jamii.Akitoa mafunzo hayo, mwezeshaji kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Stephen Mwaisobwa, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wote wanaolengwa na kampeni hiyo wanafikiwa bila kuachwa.

Alieleza kuwa watoto wote wenye umri chini ya miaka 10 watapatiwa chanjo ya matone ya Polio bila kujali kama tayari wamekamilisha au hawajakamilisha ratiba yao ya kawaida ya chanjo.“Lengo letu ni kuhakikisha kila mtoto analindwa dhidi ya ugonjwa wa Polio. Chanjo hii itatolewa kwa watoto wote waliopo kwenye umri unaolengwa ili kuzuia kabisa uwezekano wa maambukizi ya virusi vya Polio katika jamii,” alisema Dkt. Mwaisobwa.

Kwa upande wake, mwezeshaji mwingine kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Felista Kimaro, aliwahakikishia washiriki wa mafunzo kuwa chanjo ya matone ya Polio ni salama na yenye ufanisi mkubwa katika kuzuia ugonjwa huo hatari kwa watoto.Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Deograsia Mkapa, aliwataka wasimamizi wa timu za utoaji chanjo kufanya kazi kwa weledi na kujituma ili kuhakikisha zoezi la utoaji chanjo linafanyika kwa ufanisi mkubwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kulinda afya ya watoto.“Ni muhimu kila msimamizi akasimamia kikamilifu timu yake ili kuhakikisha kila mtoto anayestahili anapatiwa chanjo. Mafanikio ya kampeni hii yanategemea uwajibikaji na ushirikiano wenu,” alisisitiza Dkt. Mkapa.

Aliongeza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na wadau wa chanjo imeandaa kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone ya Polio katika Mkoa wa Geita, inayotarajiwa kufanyika kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026.Dkt. Mkapa alisema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha watoto wote waliopo kwenye umri lengwa wanapatiwa chanjo ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa Polio na kulinda afya ya jamii kwa ujumla.

Serikali imeendelea kuwahamasisha wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo muhimu mara timu za chanjo zitakapofika katika maeneo yao.

Comments