Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Doto Biteko, amewapongeza walimu wa wilaya hiyo kwa juhudi zao za kufundisha na kulea wanafunzi kitaaluma, hatua iliyochangia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao.
Pongezi hizo alizitoa hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika ngazi ya wilaya Machi 5, 2026 katika Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe. Maadhimisho hayo yalienda sambamba na kaulimbiu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi Kufikia Dira ya 2050.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Biteko alisema mafanikio ya wanafunzi katika mitihani yanaonesha juhudi kubwa zinazofanywa na walimu katika kuwafundisha na kuwaandaa wanafunzi kufikia malengo yao ya kitaaluma.
“Hii inaonesha juhudi kubwa zinazofanywa na walimu, na tunajivunia kuona wanafunzi wa kike wakifanya vizuri katika mitihani yao,” alisema Dkt. Biteko.
Aliwashukuru walimu kwa kujitoa kwao katika kuwajenga wanafunzi kitaaluma na kuwapa ujasiri wa kujiamini katika masomo yao, huku akiwahimiza walimu kuendelea kuongeza bidii ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
Aidha, aliwahimiza wanafunzi wa kike kujituma zaidi katika masomo na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuathiri malengo yao ya kielimu.
“Ninawaomba wanafunzi wa kike muendelee kujituma katika masomo yenu na kuepuka vishawishi ili kufikia ndoto zenu,” alisisitiza.
Katika maadhimisho hayo, Dkt. Biteko alieleza kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii, hivyo kuna umuhimu wa kuwaunga mkono katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo biashara ndogo ndogo, vikundi vya ujasiriamali na miradi mingine ya maendeleo.
Pia aliwataka wananchi wa Wilaya ya Bukombe kuendelea kudumisha upendo, mshikamano na uvumilivu katika familia na jamii ili kujenga mazingira bora ya malezi na maendeleo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake madhubuti na juhudi anazozifanya katika kusimamia maendeleo ya nchi, akisema hatua hizo zimemfanya kuwa miongoni mwa viongozi wanawake wanaoheshimika barani Afrika.
Alisema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi wake katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na kuimarisha misingi ya utawala bora nchini.
Aidha, aliwataka baadhi ya wananchi kuacha tabia ya kuwadharau wanawake, akisisitiza kuwa uwezo mkubwa aliouonesha Rais Samia ni ushahidi kuwa wanawake wanaweza kuongoza na kuleta maendeleo makubwa katika jamii.

Comments
Post a Comment