Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani 2026, wananchi kwa kushirikiana na wanafunzi na walimu wa Kata ya Busonzo, Kijiji cha Idoselo, wameonyesha mfano bora wa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miche 200 ya miti ya matunda katika Shule Shikizi ya Mererani.
Zoezi hilo limefanyika Machi 19, 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho hayo yenye kaulimbiu isemayo: “Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuhifadhi kwa Maendeleo ya Taifa.” Wananchi walijitokeza kwa wingi kushiriki shughuli hiyo, wakionyesha uelewa na dhamira ya kulinda rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza katika tukio hilo, Diwani wa Kata ya Businzi John Malikioli, aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanaitunza miti hiyo ili iweze kukua na kuleta manufaa ya kiuchumi na kimazingira.
“Kupanda miti ni hatua moja, lakini kuitunza ni wajibu wa kila mmoja wetu,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Emilian Fabian, aliwataka wananchi kuwa walinzi wa maliasili zao na kuachana na dhana potofu dhidi ya wahifadhi, akieleza kuwa wahifadhi wapo kwa ajili ya kulinda mazingira na siyo maadui wa wananchi.
Naye Ofisa Misitu, Bahati Kamwana, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, alitoa wito kwa wananchi kuendeleza juhudi za utunzaji wa misitu ili kuhakikisha Wilaya ya Bukombe inakuwa ya kijani na yenye mazingira rafiki kwa maendeleo endelevu.
Wilaya ya Bukombe imeendelea kufanya vizuri katika kampeni ya upandaji miti, ambapo zaidi ya miche 500,000 imepandwa katika msimu huu, hatua inayochochea uhifadhi wa mazingira na kuchangia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani hutoa fursa ya kukumbusha jamii umuhimu wa misitu kama mhimili wa uchumi, afya ya mazingira na ustawi wa maisha ya binadamu. Wananchi wanahimizwa kuendelea kupanda na kutunza miti ili kulinda mustakabali wa taifa.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, mkazi wa Kata ya Busonzo, Paul Charles, alisema elimu aliyoipata kutoka kwa wataalamu wa misitu imemsaidia kuelewa maana na umuhimu wa misitu pamoja na kazi za wahifadhi, na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wadau wa uhifadhi wa mazingira.

Comments
Post a Comment