DC ATOA SIKU 10 KUKAMILISHA UJENZI WA MADARASA SHULE YA MSINGI MNEKEZI


Na, Ernest Magashi

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Louis Bura, ametoa siku 10 kwa Kamati inayosimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Mnekezi kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa.Agizo hilo limetolewa Februari 23, 2026, wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa madarasa katika shule hiyo iliyopo Kata ya Ipalamasa, Kijiji cha Mnekezi, wilayani Chato.Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Bura amesema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji na kusisitiza kuwa ifikapo Machi 5, 2026, vyumba vya madarasa vinapaswa kuwa vimekamilika na tayari kwa matumizi ya wanafunzi.“Kamati iongeze nguvu kazi na ihakikishe upatikanaji wa vifaa vyote muhimu vya ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati,” amesisitiza Bura.Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mnekezi, Chacha Charles, amesema changamoto kubwa inayochelewesha ujenzi ni umbali wa upatikanaji wa baadhi ya vifaa, ikiwemo matofali na milango.

Ameeleza kuwa jitihada zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha vifaa vinapatikana kwa wakati na mradi huo unakamilika kulingana na maelekezo ya Mkuu wa Wilaya.

Comments