Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imefanikiwa kuvuka lengo la utoaji wa chanjo ya matone ya Polio, baada ya kuchanja watoto 189,253 dhidi ya lengo la watoto 156,777, sawa na utekelezaji wa asilimia 120.7.
Mafanikio hayo yametokana na ushirikiano thabiti kati ya wataalamu wa afya, viongozi wa serikali pamoja na mwitikio chanya wa wananchi waliotambua umuhimu wa chanjo katika kulinda afya za watoto wao.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Msimamizi wa Chanjo ya Matone ya Polio kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Stephen Mwaisobwa, aliwapongeza wasimamizi na watoa huduma za afya kwa juhudi na weledi waliouonesha katika kufanikisha zoezi hilo.
“Nawapongeza kwa kazi kubwa mliyoifanya. Mmeonyesha uwezo wa hali ya juu katika kuratibu na kusimamia zoezi hili kwa ufanisi, jambo lililoleta matokeo chanya kwa jamii,” alisema Dkt. Mwaisobwa.
Alisema zoezi hilo lilianza rasmi Machi 24, 2026 na kuhitimishwa Machi 27, 2026, likihusisha utoaji wa chanjo nyumba kwa nyumba pamoja na katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Dkt. Mwaisobwa alibainisha kuwa mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya dhati ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe katika kupambana na ugonjwa wa polio na kulinda kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, yanaendelea kuimarisha juhudi za Serikali katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki huru dhidi ya polio.
Akiwapongeza wananchi kwa mwitikio wao, aliwataka kuendelea kushirikiana na wataalamu wa afya katika kampeni zijazo ili kudumisha afya bora ya jamii na kuzuia magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.

Comments
Post a Comment