BUKOMBE YALENGA KUCHANJA WATOTO 156,777 KATIKA KAMPENI YA POLIO

Na, Ernest Magashi

Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imejipanga kikamilifu kuhakikisha watoto wapatao 156,777 wenye umri chini ya miaka 10 wanapatiwa chanjo ya matone ya Polio katika kampeni maalumu itakayofanyika kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026.Akizungumza wakati wa mafunzo kwa Kamati ya Msingi ya Afya ngazi ya Jamii (PHC), Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Deograsia Mkapa, alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika na kusisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kutoa ushirikiano ili watoto wao wapate chanjo hiyo muhimu.Dkt. Mkapa alieleza kuwa chanjo ya Polio hutolewa kwa hatua mbalimbali kuanzia mtoto anapozaliwa, ikifuatiwa na dozi za wiki ya 6, 10 na 14, huku kampeni maalumu zikiendelea kufanyika ili kuhakikisha watoto wote wanapata kinga kamili dhidi ya ugonjwa huo.“Ni muhimu kwa kila mtoto kupata chanjo wakati wa kampeni, hata kama tayari amekamilisha ratiba yake ya chanjo. Hii ni hatua ya ziada ya kuhakikisha tunadhibiti kabisa ugonjwa wa Polio,” alisisitiza Dkt. Mkapa.Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Mragili, amewataka wajumbe wa PHC na viongozi wa ngazi zote za jamii kuwa mabalozi wa uhamasishaji ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa huduma hiyo.Amesisitiza kuwa chanjo ya Polio ni salama, yenye ufanisi na hutolewa bure bila gharama yoyote, hivyo hakuna sababu kwa mzazi au mlezi kushindwa kumpeleka mtoto kupata huduma hiyo.Kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya katika kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya Polio, ugonjwa unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu kwa watoto.Wananchi wa Bukombe wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo muhimu kwa afya na mustakabali wa watoto wao. 


Comments