Askofu wa Kanisa la Ufunuo Jimbo la Geita, Rosemeri Mashauri, amewataka vijana kujishughulisha na kazi za uzalishaji mali ili kujijengea maisha bora na kuchangia maendeleo ya familia na jamii.
Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la Ufunuo Ushirombo, makao makuu ya jimbo hilo, ambapo aliungana na wanawake kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Askofu Mashauri aliwataka wazazi na walezi kuwathamini vijana na kuwapa fursa sawa za kujitafutia kipato bila ubaguzi wa kijinsia. Maadhimisho hayo yanakaulimbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi Kufikia Dira ya 2050.”
Askofu Mashauri alisema vijana wa kiume wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kukuza uchumi wao, huku akiwahimiza vijana wa kike kujituma katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, ikiwemo biashara ndogondogo, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kujenga maisha yenye mafanikio.
Katika ibada hiyo, aliwaomba pia waumini wanawake kuendelea kuwaombea viongozi wa Serikali, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Doto Biteko, ili Mungu aendelee kuwalinda na kuwaongoza wanapoendelea kuwatumikia wananchi kupitia Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Askofu Mashauri aliwahimiza wanawake kuendelea kushikamana na kuwasaidia watu wenye uhitaji katika jamii, akisisitiza kuwa kufanya matendo mema ni mapenzi ya Mungu na huleta baraka katika maisha ya mwanadamu.
Pia aliwataka wanawake kuendeleza malezi bora ya maadili na utamaduni wa Kitanzania, hatua itakayosaidia kujenga familia imara na jamii yenye misingi ya maadili mema yanayompendeza Mungu.
Kwa upande mwingine, aliwakumbusha wanaume kutokutelekeza familia zao wanapokumbana na changamoto za kifamilia. Badala yake, aliwashauri kushirikisha ndugu wa karibu pamoja na viongozi wa dini ili kusaidia kutatua migogoro na kudumisha amani katika familia.
Vilevile aliwahimiza wanaume kuwaruhusu wake zao kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali, akieleza kuwa hatua hiyo husaidia kuongeza kipato cha familia na kuchangia maendeleo ya taifa. Alisisitiza kuwa wanawake wasidhalilishwe kwa majina kama “mama wa nyumbani” au “golikipa”, bali waheshimiwe kwa mchango wao katika maendeleo ya familia.
Askofu Mashauri pia alieleza kuwa kabla ya kufikia kilele cha maadhimisho ya Machi 8, 2026, wanawake wa Kanisa la Ufunuo walitembelea Gereza la Wanawake Machi 6,2026 na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kama sehemu ya matendo ya huruma kwa jamii.
Akizungumza baada ya ibada hiyo, mmoja wa waumini, Magireti Paul, alimshukuru Askofu Mashauri kwa mafundisho aliyoyatoa, akisema yamempa moyo na ujasiri wa kutambua kuwa wanawake wana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi licha ya changamoto za ubaguzi zinazojitokeza katika jamii.
Naye Neema Joel alisema mafundisho hayo yamempa hamasa ya kuanza kujishughulisha na shughuli za kiuchumi badala ya kusubiri msaada. Alisema ana mpango wa kuanzisha biashara ndogondogo ya kuuza mboga mboga ili kujipatia kipato na kuboresha maisha yake.
Ujumbe wa Askofu Mashauri ulisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia, bidii katika kazi na mshikamano wa kifamilia kama msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.

Comments
Post a Comment